Tahariri: Tunahitaji mikakati madhubuti kutokomeza sifuri na daraja la IV kidato cha nne Tanzania

January 10, 2020 9:07 am · Mhariri
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Januari 9, 2020 lilitangaza matokeo ya mitihani ya kujipima ya darasa la nne, kidato cha  pili na ile ya kuhitimu kidato cha nne iliyofanyika mwishoni mwaka jana.

Hata hivyo, kati ya matokeo yote hayo, yaliyogusa wengi zaidi ni matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

Necta imesema ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kidogo kwa asilimia 1.4 kutoka ule wa mwaka 2018.

Necta imeeleza kuwa katika mtihani huo wanafunzi 340,914 wamefaulu kati ya wanafunzi 422,722 waliofanya mtihani ikiwa ni sawa na takriban asilimia 81 ya watahiniwa wote.

Licha ya ufaulu huo kuongezeka, bado takriban nusu ama asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa mwaka 2019 wamepata daraja la nne ikiwa ni sawa na watahiniwa 205,613.  Ni theluthi tu ama asilimia 32 ya watahiniwa wote wa mwaka jana ndiyo walipata daraja la kwanza hadi la tatu (I-III) au sawa na wanafunzi 135,301.

Takwimu hizo za Necta zinabainisha zaidi kuwa watahiniwa 81,808 au sawa na asilimia 19 ya waliofanya mtihani huo wamefeli. Hii ni sawa na kusema watoto 19 kwa kila 100 wamefeli.

Pamoja na kuongezeka kidogo kwa ufaulu kwa mtihani huo wa mwaka jana, bado tunaona kama Taifa tunatakiwa kujifunga mkanda kuongeza ufaulu wa watoto hao zaidi ya sasa. Ufaulu huo uende ndani zaidi katika ubora wa ufaulu.

Kwa sasa Taifa linahitaji vijana wenye ufaulu mzuri wa wastani wa daraja la I hadi la III na wenye maarifa bora ya kuwawezesha kukabiliana na changamoto zinazowakabili zikiwemo za ukosefu wa ajira na siyo daraja la IV na waliofeli.

Kitendo cha matokeo ya mwaka 2019 kuwa na takriban nusu ya wanafunzi wenye daraja la IV na wengine asilimia 19 kufeli siyo kizuri licha ya kuwa ufaulu wa jumla umepaa.

Kama tunavyofahamu baadhi ya wanafunzi waliomo kwenye daraja la IV huenda wakashindwa kushindana katika fursa za kujiendeleza na masomo hata ya ngazi ya cheti. Wale waliofeli ndiyo kabisa huwa hawana vyeti ambavyo vinaweza kuwasaidia kujiendeleza kielimu zaidi hata katika baadhi ya mafunzo ya ufundi.

Ili kutengeneza vijana wanaoweza kukabiliana na changamoto za karne ya 21, hatuna budi kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza maarifa ya kuishi na jamii.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo wenye mapenzi mema hawana budi kuwekeza zaidi katika kuongeza vyumba vya madarasa, walimu bora, vitabu, na vifaa vingine muhimu vya kufundishia katika shule za umma ambazo zimeonekana kutofanya vizuri kuliko za binafsi. 

Muhimu kuliko yote, Serikali iwekeze vilivyo katika kuboresha maslahi ya walimu ili wapate hamasa ya kufundisha vema.

Mbali na masuala ya darasani, tunashauri wanafunzi pia wafundishwe nidhamu, kupenda na kuheshimu kazi, kuwa tayari kujifunza na ujasiri wa kukabiliana na changamoto. Madaraja I au II hayatakuwa na msaada maishani mwao iwapo hawatakuwa na nidhamu, maarifa nje ya yale ya darasani.

Uwekezaji wa namna hii siyo tu utaongeza ufaulu, bali utatengeneza vijana wanoweza kuishi mahali popote duniani wakisaka fursa mbalimbali za maendeleo.

Kila mmoja wetu kwa nafasi yake kuanzia Serikali, wazazi na walezi, walimu na wadau wengine tunaweza kufanya jambo na kuwasaidia vijana hawa kujiendeleza kielimu na kuwa tayari kukabiliana na changamoto za maisha.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW