Soko la pilipili kichaa lashuka kwa miezi mitano mfululizo Tanzania

December 20, 2022 11:38 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
  • TAHA yaahidi kuwatafutia masoko wakulima. 

Dar es salaam. Wakati bei ya mazao ya chakula kama mahindi na mchele  yakiendelea kupanda katika baadhi ya maeneo nchini, hali si shwari kwa wafanyabiashara wa zao la pilipili kichaa baada ya mwenendo wa soko la  zao hilo kutokuwa wa kuridhisha kwa siku za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Maendelo ya Tasnia ya Mazao ya mboga, matunda na Viuongo Tanzania Horticulture Association (TAHA), kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa zao la pilipili kichaa (African Bird Eye Chili) kutokana na fursa kubwa za masoko hasa ya nje katika nchi za Hispania na Urusi.

Hata hivyo, TAHA katika taarifa yake iliyotlewa Novemba 17 mwaka huu imeeleza kuwa mwenendo wa soko wa zao hilo umekuwa ukishuka kwa miezi mitano mfululizo kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

“Vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine iliyoanza mwanzoni mwa mwaka 2022, imesababisha kuvurugika kwa sekta ya usafirishaji na ugavi hasa katika Bara la Ulaya. 

“Hivyo, wanunuzi wengi wa kimataifa wameshindwa kufikia masoko yao kwa haraka na kwa uhakika, na kupunguza ununuzi wa bidhaa mbalimbali ikiwemo pilipili kichaa,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya mwaka 2022 Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema Wizara itahamasisha uzalishaji wa zao la pilipili kichaa kutoka tani 7,270 mwaka 2018/19 hadi tani 7,561 mwaka 2022/23.


Soma Zaidi

TMA yataja sababu ongezeko la joto baadhi ya mikoa Tanzania


Hataua zinazochukuliwa

Kutokana na changamoto hiyo, TAHA kwa kushirikiana na wadau wengine imeeleza kuwa inafanya jitihada za kutafuta masoko mbadala ya ikanda ikiwemo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kufanya tathmini ya kina ya kiwango ambacho hakijanunuliwa na kukitafutia wanunuzi, kuwashauri wakulima mazao mbadala yatakayothibitika kuwa na uhitaji kwenye soko pamoja na kuandaa kongamano maalumu.

“Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, tutaandaa mkutano wa wadau wa zao la pilipili utakaojumuisha wadau wote muhimu kutoka sekta za umma na binafsi ili kujadili mikakati ya kuendeleza zao hili hususan upatikanaji wa masoko, ubora wa mazao, pamoja na uongezaji thamani (Value Addition),” inasomeka taarifa hiyo.

Licha ya kutumika kama kiungo cha chakula pilipili kichaa hutumika kama malighafi ya kutengenezea bidhaa za viwandani kama mabomu ya machozi, dawa za kuchua misuli pamoja na rangi za kupaka midomoni.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW