Rais Samia amtumia salamu Rais Putin, Urusi ikiadhimisha Siku ya Ushindi

May 9, 2025 4:36 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema siku hiyo hiyo inabeba ushujaa, ustahimilivu na kujitolea kwa wananchi wa Urusi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, pamoja na wananchi wa nchi hiyo wanaoadhimisha Siku ya Ushindi, tukio muhimu linalokumbukwa kwa ushindi wa Urusi dhidi ya Ujerumani ya Nazi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Rais Samia kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii za Instagram na X (Zamani Twitter) amechapisha salamu hizo ambapo amesema siku hiyo inabeba ushujaa, ustahimilivu na kujitolea kwa wananchi wa Urusi.

 “Napenda kutoa pongezi zetu za dhati kwako katika kuadhimisha Siku ya Ushindi, siku adhimu inayobeba maana ya ushujaa, ustahimilivu na kujitolea kwa wananchi wa Urusi katika harakati za kupigania uhuru na amani,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa kumbukumbu ya siku hiyo inaendelea kuhamasisha mataifa duniani kote kuthamini na kudumisha amani na haki kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwanini siku hii ni muhimu kwa Urusi

Siku ya Ushindi huadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Mei, kama kumbukumbu ya siku ambayo Ujerumani ya Nazi ilikubali rasmi kushindwa mwaka 1945, na hivyo kumaliza rasmi Vita Kuu ya Pili ya Dunia katika Bara la Ulaya. 

Kwa Warusi, siku hii ni alama ya mshikamano wa kitaifa, ujasiri wa wanajeshi na raia, pamoja na urithi wa kihistoria unaothaminiwa kwa vizazi mbalimbali na huadhimishwa kwa gwaride kubwa la kijeshi na huhudhuriwa na viongozi wa mataifa mbalimbali ambapo mwaka huu Rais wa China Xi Jin Pin na Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ni miongoni mwa waliohudhuria.

Tanzania na Urusi zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu tangu enzi za harakati za ukombozi barani Afrika, ambapo Urusi ilitoa msaada mkubwa kwa mataifa mbalimbali ya Kiafrika katika jitihada zao za kujikomboa kutoka kwa ukoloni.

Wakati wa enzi ya vita baridi, Tanzania chini ya uongozi wa Julius Nyerere, ilifuata sera ya kutofungamana na upande wowote, ikisaka msaada kutoka nchi za Magharibi na Mashariki.

Umoja wa Kisovieti, sasa Urusi, uliiona Tanzania kama mshirika muhimu barani Afrika na kutoa msaada katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na miundombinu, elimu na ulinzi.

Nchi hizi mbili zimeimarisha ushirikiano wao kupitia diplomasia ya kiuchumi. Picha | Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.

Ushirikiano huo uliongezeka zaidi kutokana na mwelekeo wa kisoshalisti wa Tanzania na msimamo wake dhidi ya ukoloni wakati wa vita baridi, ambao ulilingana na malengo ya Sera za kigeni za Urusi.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizi mbili zimeimarisha ushirikiano wao kupitia diplomasia ya kiuchumi ambapo Tarehe 28 Oktoba 2024, Tanzania na Urusi zilisaini makubaliano muhimu katika kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakati wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Mbaga Kida, alieleza kuwa ushirikiano huo unalenga kukuza fursa za kiuchumi kupitia sekta za kilimo biashara, madini, utalii, afya na elimu. 

Kwa upande wake Pavel Kalmychek kutoka Wizara ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Urusi alisisitiza kuwa ushirikiano huo utafungua njia mpya za maendeleo kwa pande zote mbili, huku Urusi ikionesha utayari wa kushirikiana katika maeneo yote yaliyoafikiwa.

Urusi inafanya maadhimisho hayo huku ikiwa ni miaka mitatu tangu ianze kufanya kile inachokiita oparesheni ya kijeshi nchini Ukraine jambo lililoitumbukiza dunia katika mgogoro wa kiuchumi uliokuwa unapona majeraha ya janga la Uviko-19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks