Sio kweli ni uzushi, Gen Z Kenya wakivuta moshi wa bomu la machozi

July 9, 2024 1:42 pm · Daniel Mwingira
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Kutokana na maandamano yanayoendelea nchini Kenya, habari nyingi za uzushi zimekuwa zikisambaa sehemu mbalimbali, zikihusisha picha na video na wakati mwingine  zimekuwa zikisambazwa na mashirika makubwa ya habari katika sehemu za Afrika, hususan Afrika Mashariki.

Mathalani video iliyosambaa hivi karibuni ikiwaonesha vijana waandamanaji nchini Kenya maarufu kama ‘Gen Z’ wakivuta moshi bomu la machozi, jambo ambalo halina ukweli wowote.

Habari hiyo iliyochapishwa na Televisheni ya The Citizen Nchini Kenya imeripotiwa pia na vyombo vya habari vingine ikiwemo vya nchini Tanzania kama Millard Ayo na Tupo Media,


Soma zaidi: Debunked: Kenyan MP’s did not eat in the bush following bill protest


Katika video hiyo kijana aliye katika maandamano ya Gen Z nchini Kenya alishikilia bomu la machozi lenye rangi ya bluu na njano, huku akionekana kulivuta kama mtu anavyovuta sigara.

Mwandamanaji huyo alisikika akisema bomu hilo ni la pilipili, sasa anataka la ‘strawberry’, na kwenye video hiyo anasikika akisema, “lete ya strawberry, hii ni ya pilipili,” kisha anaonekana akimpa mwandamanaji mwingine na yeye akilivuta.

Ukweli huu Hapa!

Utafiti mdogo uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa si kweli kuwa mwandamanaji huyo anavuta bomu hilo la machozi licha ya kuonekana akilivuta katika video hiyo.

Huenda bomu hilo la machozi lilishatoa gesi yake yote hivyo mwandamanaji huyo aliweza kulitumia kama chombo cha kawaida.

Ukitazama video hiyo vizuri utagundua bomu hilo lina matundu kwenye kopo ambayo ndiyo yanayosaidia kutoa moshi ambapo kijana huyo aliyatumia kuingiza sigara.

Tukio hilo lililotokea katika mji wa Nyeri linaonyesha kijana huyo akiweka sigara ndani ya kopo hilo la bomu la machozi, huku mkono mwingine ukiwa umeshikilia kiberiti cha kuwashia moto.

Pia habari hiyo imeshafanywa na mashirika  kama RTR Afrika ambao pia wamethibitisha kuwa sio kweli.

Kwa hiyo, si kweli kuwa kijana huyo alikuwa anavuta moshi wa bomu la machozi, bali ni kopo la bomu lililokuwa limeishatoa moshi wake.

Enable Notifications OK No thanks