Simulizi ya mcheza ngoma aliyeng’atwa na nyoka zaidi ya mara 10-2

February 8, 2022 6:03 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Nyoka hutumiwa kunogesha ngoma na kuvutia watu wengi.
  • Ili kuepuka kung’atwa na nyoka unatakiwa kucheza naye kwa akili. 

Mwanza. Baada ya kupata kisa cha mwalimu wa ngoma za asili, Thobias Gwende kung’atwa na nyoka zaidi ya mara 10, makala hii inakufahamisha kwa kina mambo ya kuzingatia wakati wa kucheza na ngoma.

Matamasha ya utamaduni yanayofanyika Tanzania yamekuwa sehemu muhimu ya kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi za Watanzania. Pia hutumika kutangaza utamaduni huo kwa wageni kutoka nje ya nchi.

Matamasha hayo ambayo hufanyika katika ngazi mbalimbali za kitaifa yamekuwa yakipambwa na shughuli tofauti tofauti ikiwemo ngoma, nyimbo za asili, maonyesho ya mapishi na michezo ya makabila.

Hata hivyo, karibu matamasha yote unayoweza kuhudhuria, utakutana na mnyamapori nyoka ambaye hutumika kunogesha burudani ya ngoma na muziki.

Kwa sababu siyo kawaida nyoka kuonekana katika mazingira ya kawaida, wanamuziki wa nyimbo za asili wanaotumbuiza humtumia nyoka kama kivutio cha watu.

Kinachowavutia ni kushuhudia binadamu anavyoweza kuwa karibu na nyoka halafu asipate madhara, ikizingatiwa kuwa mnyama huyo amekuwa akiogopwa na watu wengi kwa sababu ya sumu aliyonayo ambayo husababisha kifo ikiwa atamng’ata mtu.

Baadhi ya wacheza ngoma wakiwa katika picha ya pamoja katika moja ya tamasha la ngoma asili mkoani Mwanza. Picha| Thobias Gwende.

Sababu za kutumia nyoka katika michezo ya ngoma

Mwalimu wa ngoza za asili nchini, Thobias Gwende anasema nyoka hutumika kunogesha ngoma na nyimbo na hivyo kuvuta watu wengi kuwatazama.

“Wasanii hupenda kutambiana kuonyesha majigambo, hivyo kundi hili litambia mwezake kuwa anaweza kucheza kuliko mwenzake,” anasema  Gwende.

Gwende anasema nyoka huvuta watu wengi kwa sababu watu wanaamini mnyama huyo hawezi kuwa karibu na binadamu. 

Baadhi ya ngoma za maarufu Kanda ya Ziwa ambazo zimekuwa zikisifika kumtumia nyoka katika shughuli zao ni pamoja na Bugobogobo,  Wayeye na Wanungule. 

Si jambo jepesi kwa watu kumkamata nyoka na kuanza kucheza naye lakini kwa wasanii wa ngoma za asili hususani Wayeye wao wanamudu  kucheza na mnyama huyo hatari.

Gwende anasema hutumia njia mbalimbali kuwapata nyoka msituni ili kuwatumia katika shughuli za ngoma baada ya kupata kibali kutoka serikalini.

Hutumia mti unaojulikana kwa jina ngamba ambao hukatwa na kuchongwa kwa mfano wa kalai na baada ya hapo huwekewa maji ambayo huchanganywa na dawa mbalimbali kisha wazee maarufu na wasanii huingia msituni na vifaa hivyo ili kuwapata nyoka. 

“Inahitajika  imani lakini pia ili zoezi lifanikiwe  wazee hutumia dawa mbalimbali ambazo huchangany’wa na maziwa freshi ambapo mzee maarufu huyameza mdomoni kisha kuanza kuomba kwa kupuliza akizunguka pande zote za dunia ili jambo lao lifanikiwe,” anasema mwalimu huyo ngoma ambaye anaweza kucheza karibu ngoma zote za makabila ya Tanzania. 

Baada ya tukio hilo la kimila, nyoka wa aina zote hufika kwenye mti huo uliochongwa kwa mfano wa karai kisha kunywa maji yaliyomo ambayo huwalegeza,  jambo linalowapa wepesi wa kuchagua aina ya nyoka wanayemhitaji.

Nyoka husika huchukuliwa na kutunzwa sehemu salama na hutumika katika matamasha mbalimbali. 


Soma zaidi: 


Aina ya nyoka wanaotumika zaidi?

Nyoka aina ya chatu ndiyo hutumika zaidi katika shughuli muziki na ngoma za asili. Chatu ni nyoka ambaye anadaiwa kuwa na sifa ya upole na hawezi kusababisha madhara makubwa kwa binadamu bila kumchokoza.

Gwende anasema wasanii wa ngoma za Kisukuma walichagua kumtumia nyoka huyo kutokana na sifa hiyo ingawa pia chakula anachotumia kinaweza kupatikana kirahisi na anaweza kufugika kuliko nyoka wengine akiwemo koboko.

Inaelezwa kuwa  chatu anaweza kula vumbi la udongo wa mfinyanzi unaoweza kuchanganywa na unga wa udaga. Pia anaweza kula sungura na kuku.

“Cha kufanya tu wakati unampelekea kuku au sungura hupaswi kumpelekea mzoga hataweza kula anahitaji  aliyevhai ili aweze kumfukuza mwenyewe amkamte ndipo amle, ukimpeleka aliyekufa hatamla kwavkuwa atahofia kuwa umempelekea sumu,” anasema Gwende.

Sifa nyingine ni kuwa nyoka huyo ni mkubwa na kwamba hata sumu yake siyo kali kama wengine kwa kuwa mtu anaweza kuishi na sumu hiyo kwa muda wa saa 24 akimng’ata.

Namna ya kucheza na nyoka usipate madhara

Si jambo la kawaida  lakini kwa  wasanii wa ngoma za asili hasa Wasukuma mara nyingi utawakuta wakicheza na wanyama hao hatari kwenye sherehe mbalimbali.

Wasanii hao hukusanya makundi makubwa ya watazamaji ambao humiminika kushuhudia umaridadi mkubwa wa wachezaji hao wanavyoonyesha mbwembwe zao wakati wa kucheza na wanyama hao.

Kwa mujibu wa Gwende, ili waweze kucheza vizuri na nyoka wanamkata kucha mbili ambazo ziko sehemu ya mkia ambazo zina ncha kali kama sindano ambapo zikimchoma mtu zinatoa sumu kali kuliko hata meno.

“Tunachokifanya sasa ni kuzikata zile kucha ili kumpunguzia makali kisha yule anayecheza hupakwa na kuchanjwa dawa ambayo humwongezea ujasiri wa kumkamata huyo nyoka kisha kucheza naye,” amesema Gwende

Anasema msanii anatakiwa kumshika nyoka kichwa na mkia ili kuzuia asijikunje na endapo ukikosea katika kumshika anaweza kumng’ata.

“Aababu nyingine inayochAngia nyoka akung’ate ni magamba yake huwa yanatekenya misiri ya kitu kina kutembea mwilini , hisia hizo zinaweza kukusababisha ukamwachia kichwa na kumpa nafasi ya kukung’ata,” anasema Ngwende

Inapotokea nyoka amekung’ata hutakiwi kumtoa mwache hadi amalize kisha atatoka mwenyewe na baada ya hapo kuna dawa huwekwa sehemu hiyo kuzuia sumu isisambae lakini pia kuruhusu meno kutoka ambapo inachukua dakika 15 hadi 20 maumivu yanakuwa sawa, anaeleza Gwende. 

Mila hizo zinarithishwa kwa vizazi vijavyo?

Mtemi wa kabila la Wasukuma Mkoa wa Mwanza, Charles Itale anasema pamoja na ngoma hizo kufurahisha watazamaji lakini pia zinachochea utalii wa ndani.

“Bado watu hawaamini kama kuna wacheza ngoma wanaweza kucheza na nyoka hivyo wanataka kwenda kushuhudia kama ni kweli na namna wanavyoweza kucheza hivyo hiyo inahamasisha utalii wa ndani,” anasema Itale.

Mtemi huyo (78) anasema kinachofanyika kwa sasa ni kujaribu kuhamasisha vijana kuenzi na kuendeleza mila na tamaduni zao ikiwemo kucheza ngoma za asili kwa kutumia nyoka.

“Changamoto kubwa hapa ni mwingiliano baina ya pande na makabila ya watu tofauti tofauti, hali hiyo inasababisha watoto washindwe kujua tamaduni zao halisi hivyo kuiga mambo ya kigeni,” anasema Itale 

Anasema viongozi wa mila mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali wameanza kuandaa matamasha yatakayosaidia kurudisha mila na tamaduni za kiafrika.

“Mifumo ya kimaisha imechangia mila hizi kusahaulika zamani ngoma za asili zilichezwa kwenye sherehe mbalimbali mfano Bulabo, harusi, mavuno, mtu kupanda cheo na kulikuwa na maandalizi makubwa ambapo jamii ilichangia michango ya chakula na zawadi ambazo zingetolewa kwa wasanii hao,” anasema Itale.

Mtemi Itale anasema umefika wakati ambao Jamii inapaswa kuhakikisha inarithisha mila hiyo huku wazazi wakishauriwa kuwafundisha watoto lugha za kwao na mila za kwao ili kurejesha utamudini wa Waafrika.

Enable Notifications OK No thanks