Simu inavyoweza kuimarisha ulinzi nyumbani, ofisini

May 29, 2020 2:42 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Unahitaji kuwa na simu mbili au zaidi na kupakua programu za kamera kwenye simu hizo.
  • Utachagua simu moja kuwa skrini na nyingine kutumika kama kamera.
  • Weka katika maeneo ambayo unapenda ili kufuatilia mwenendo wake. 

Dar es Salaam. Kuna wakati mwingine unahitiji kuwa na ulinzi wa ziada kwenye eneo lako la kazi na hata nyumbani ili kuongeza usalama wa watu na mali zako. 

Huenda unatamani kufunga kamera maalum za ulinzi (CCTV Camera) lakini mfuko wako hauruhusu. Simu yako inaweza kukusaidia kutimiza kusudi hilo la ulinzi nyumbani. 

Simu hasa zile janja zina kamera ambayo ikitumika vizuri inaweza kurekodi matukio yote ya nyumbani na kukuwezesha kujua nini kinaendelea hata kama haupo.  Haya ndiyo mambo unayohitaji kufanya ili kufanikisha hatua hiyo:

1. Pakua kamera ya ulinzi kwenye simu 

Kuna programu nyingi kwenye maduka ya mtandaoni lakini kwa kuanzia, unaweza kuchagua programu ya “Alfred” ambayo inapatikana kwenye duka la  Play Store na hata App store kwa simu za iPhone.

Mbali na Alfred, zipo programu za Manything, Salient Eye na Presence. 

Baada ya kuipakua, anzisha programu hiyo na kisha soma utambulisho wa programu hiyo.

Kwenye simu ambayo unataka ifanye kazi kama kamera, hakikisha unachagua “Camera” baada ya kumaliza utambulisho wa programu. Na kwa simu ambayo utaitumia kama skrini ya kuangalizia, chagua “Viewer”. Baada ya hapo bonyeza “Next” (yafuatayo).

Utatumia simu moja kama kamera na nyingine kama skrini ya kuangalizia kinachoendelea. Picha| reviews.com

Baada ya hapo unaweza kukamilisha usajili kwa kuingiza taarifa zako za akaunti ya Google. Hakikisha unatumia akaunti moja kwenye simu zote.

Unaweza kuongeza manjonjo kwa kuwasha mifumo kama kung’amua miondoko (movement), kuruhusu na kuondoa sauti na pia kuchagua kamera ipi unataka kutumia yaani kama ni ya nyuma au ya mbele.

2. Chagua eneo la kuweka kamera yako

Kama ni kwa ajili ya ulinzi ni hakika hautapenda ionekane kwa urahisi. Unaweza kuielekeza kamera hiyo kwenye maeneo muhimu kama kwenye mlango wa kuingilia nyumbani au sehemu unapohifadhi vitu vyako vya thamani.

Kama una simu nyingi, unaweza kuziweka popote unapohitaji ili uweze kuona sehemu nyingi kwa wakati mmoja.


Zinazohusiana


3. Jinsi ya kuweka na kuanza matumizi

Kwa kuwa ni simu, ni dhahiri kuwa inahitaji kuwa karibu na eneo la chaji kwani itakuwa ikifanya kazi kwa muda mwingi hivyo kukupatia ulazima wa kuiweka karibu na eneo ambalo chaja yake inaweza kuifikia kirahisi. 

Pia unaweza kuchagua kununua waya wa kuchajia mrefu ili upate machaguo mengi zaidi.

Ili kuiweka ikae vizuri, unaweza kutafuta eneo zuri la kuitegesha au kununua vifaa maalumu vya kushikia simu.

Baada ya hapo, unaweza kufungua programu yako kwenye simu yako na ukaanza kuangalia kinachoendelea.

Kwa kutumia njia hii itakuwa ni rahisi kufuatilia mienendo ya mtoto mdogo nyumbani na hata mgonjwa ambaye yupo nyumbani bila mwangalizi ambapo unaweza kuona kitu kinachoendelea nyumbani mubashara kutoka popote ila tu uwe umeunganishwa na intaneti

Programu hiyo inakuja na uhifadhi wa video zitakazochukuliwa hivyo ni vizuri kuhakikisha kuwa simu unayotumia ina nafasi kubwa ya kuhifadhi kumbukumbu au kuhamishia katika vifaa vingine vyenye uwezo mkubwa. 

Ni rahisi pia kufuatilia sehemu yako ya biashara hasa kama ni kubwa na inahitaji uangalizi mkubwa.

Endelea kusoma Nukta kwa teknolojia rahisi ambazo zimekuwa zikikusubiri kuzitumia.

Enable Notifications OK No thanks