Rais Samia azindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, atoa mwelekeo kwa Serikali, sekta binafsi

July 17, 2025 5:23 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema ili kufikia malengo ni lazima kuwe na mabadiliko ya fikra, utendaji kazi pamoja na mifumo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema ili nchi ifikie malengo iliyojiwekea katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,  taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi wanapaswa kuwa na mabadiliko ya fikra, utendaji kazi pamoja na mifumo.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na Watanzania katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dodoma leo Julai 17, 2025, amesema dira hiyo inalenga kuifikisha Tanzania katika ngazi ya uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.

Rais Samia amesema lengo hilo litafikiwa kwa kufikia pato la Taifa la Dola Trilioni moja za Marekani na pato la mtu mmoja mmoja la zaidi ya Dola 7,000 za Marekani kwa mwaka.

“Hatutoweza kufikia lengo hili kama tutaendelea kufanya kazi kwa mazoea. Lazima tubadilike kifikra, kimtazamo na kimatendo. Vile vile lazima tupimane kwa matokeo ya kazi,” ameeleza Rais Samia.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Jijini Dodoma. Picha Maelezonews.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) Tanzania kwa sasa ni nchi ya kipato cha kati cha chini, ikiwa na pato la taifa kwa mtu mmoja (GDP per capita) la Dola za Marekani 1,149 sawa na Sh2.9 milioni. 

Katika kuhakikisha utekelezaji wa dira hiyo, Rais Samia ameielekeza Tume ya Taifa ya Mipango, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kuandaa nyenzo zitakazopima utendaji wa serikali kulingana na malengo ya dira. 

Ameagiza pia sera zote za wizara zipitiwe na kurekebishwa kabla ya utekelezaji kuanza rasmi Julai 2026.

Rais pia ameitaka Tume hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza mchakato wa kuchambua na kupendekeza maboresho ya kisheria ili kuwezesha utekelezaji wa dira.

Aidha, mfumo wa ufuatiliaji na tathmini umetajwa kuwa kipaumbele katika kuhakikisha taasisi zote za umma zinapimwa kwa vigezo maalum vinavyolingana na malengo ya dira.

Rais Samia  ameelekeza pia taasisi za Serikali kuwa na viashiria vya utendaji vinavyoendana na dira hiyo.

Kwa upande wa sekta binafsi, Rais Samia amesema mafanikio ya dira hayawezi kufikiwa bila ushiriki wa dhati wa sekta hiyo ambapo ameitaka sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maeneo ya kiuchumi, uwekezaji, ubunifu, uundaji wa ajira zenye staha na kuongeza tija.

“Sekta hii nayo ijipange vyema… utekelezaji wa dira 2050 unahitaji ushiriki wa kimkakati kutoka kwa sekta binafsi,” amesema Rais Samia.

Awali, mfanyabiashara Rostam Aziz aliyekuwa akiongea kwa niaba ya sekta binafsi ameiomba Serikali kuweka mkakati maalumu wa kuijenga nakuilinda sekta binafsi ya ndani.

“Watanzania ndio watakaoijenga nchi yao ni lazima wawekezaji wa ndani wapewe fursa na kulindwa. Tuvilinde sana viwanda vyetu vya ndani kwani hakuna nchi iliyofanikiwa katika kujenga uchumi wake bila kuwa na viwanda,” amesema Aziz.

Katika kuhakikisha ushirikishwaji mpana, Rais ameagiza kuwepo kwa mkakati wa mawasiliano na uelimishaji kwa umma kuhusu dira hiyo ili kila mdau aelewe nafasi yake.

Kuhusu upatikanaji wa haki, Rais Samia ametoa wito kwa Mahakama na taasisi zinazohusika kuhakikisha kila mtu anapata haki anayostahili.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo amesema dira hiyo inaangazia maeneo manne makuu ambayo ni ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii, utawala bora na utunzaji wa mazingira.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Picha /Maelezonews.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma tarehe 17 Julai, 2025.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Fred Msemwa amesema dira hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na wananchi, ambapo zaidi ya watu milioni 1.174 walishiriki moja kwa moja kwa kujaza madodoso na kutoa maoni.

Rais wa TanzaniavSamia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.Picha/ Ikulu Mawasiliano.

Katika uteuzi wa sekta za kimageuzi, Rais Samia amesema zitachaguliwa kwa kuzingatia uwezo wa kuzalisha ajira, kuongeza mauzo ya nje, kuchochea sekta nyingine, kuongeza thamani ya mazao, na kukuza mapato ya Serikali.

Sekta hizo ni pamoja na kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, madini, uchumi wa buluu, michezo, ubunifu wa huduma za kifedha na huduma kwa ujumla.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa Tanzania unaolenga kuhakikisha nchi inafikia viwango vya juu vya maendeleo ifikapo mwaka 2050. 

Dira hii inalenga kuimarisha maeneo mbalimbali ya kiuchumi, kijamii, na kimazingira ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi na kufikia uchumi wa kati wa juu.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
25 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
25 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV