Si kweli: video zinazoonesha mnyama wa baharini mwenye kichwa cha ng’ombe

July 11, 2024 9:07 am · Daniel Mwingira
Share
Tweet
Copy Link
  • Nukta Fakti ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa picha hizo zimetengenezwa na kuhaririwa kwa kutumia akili ya bandia (AI).

Dar es Salaam. Kumekuwa na video inayoonesha mnyama mwenye kichwa cha ng’ombe na mapembe, na kiwiliwili cha mnyama mwingine wa baharini ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ndani na nje ya Tanzania. Hata hivyo, video hiyo si ya kweli.

Madai ya video hiyo kuwa ni kiumbe cha ajabu

Video hiyo haina sauti wala maelezo, lakini inaonyesha mnyama huyo akitoa sauti kama ya ng’ombe huku akizungukwa na watu. 

Hata hivyo, video hiyo haionyeshi sura za watu hao. Pia, kuna video nyingine yenye kichwa cha habari ‘Sea Cow’ iliyo na maneno kwa lugha ya Kiingereza ‘is really scaring’ ikimaanisha kuwa kiumbe hicho ni cha kuogofya.

Ukweli Huu Hapa!

Kutokana na uchunguzi wa Nukta Fakti, ilibainika kuwa picha hizo zimetengenezwa na kuhaririwa kwa kutumia akili ya bandia (AI). Licha ya video hiyo kuonyesha tu mnyama huyo na mikono na miguu ya watu, kuna mambo kadhaa yanayoonyesha picha hizo ni za kutengenezwa kutokana na kuonekana kwa vitu visivyo vya kawaida.

Kwa mfano, picha moja inaonyesha hali isiyo ya kawaida kwenye mikono ya watu waliokuwa wakimshangaa mnyama huyo, kuna walioonekana kuwa na mikono iliyoungana na kuingiliana, hali ambayo inatilia shaka video hiyo kuwa huenda imetengenezwa au kuhaririwa kwa msaada wa akili ya bandia (AI).

Kitu kingine cha kutilia shaka kwenye video hiyo ni miondoko ya mtu kuanzia sekunde ya tatu ndani ya video hiyo  inayoonyesha mtu mwenye  miguu mitatu, ambapo mguu mmoja unaelekea mbele na miwili nyuma. Jambo hili ni la kutilia shaka kwa kuwa ni nadra sana kukutana na binadamu kama huyo. 

Swali la msingi la kujiuliza ni imekuwaje katika video hiyo ya mnyama anayefanana na ng’ombe yeye kuwa kiumbe cha ajabu, lakini hata hao watu wanaomzunguka nao wanaonekana kuwa na maumbile ya ajabu kama mi

guu mitatu na mikono kuungana. Hali hiyo inatosha kuthibitisha kuwa video hiyo inaweza kuwa sio ya kweli bali ni ya kutengenezwa.

Mfahamu ngombe bahari

Kwa mujibu wa tovuti ya wanyama ya BBC, ngombe bahari ni miongoni mwa viumbe maji wanaoishi na kuzaliana majini wakiwa na urefu unaokadiriwa kuwa mita tatu na uzito wa hadi kilo 145.

BBC inafafanua kuwa wanyama hao wenye pua kubwa na macho madogo hupatikana zaidi katika maziwa bahari na chakula chao kikuu ni magugu na majani ya baharini.

Kama ilivyo kwa wanyama wengine wa baharini kama kiboko, ng’ombe bahari huweza kuishi nchi kavu kwa muda mchache.

Enable Notifications OK No thanks