Si kweli: TEC imetoa waraka kuhusu Uchaguzi Mkuu 2025
- TEC imesema haihusiki na maudhui yeyote yaliyopo kwenye waraka huo feki na inasisitiza waumini na watanzania kuupuuza.
Dar es Salaam. Huenda ukawa ni moja ya watu waliokutana na chapisho katika mitandao ya kijamii linalodaiwa kuwa ni waraka uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) likitoa msimamo wa baraza hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.
Chapisho hilo feki limesambaa likiwa na nembo na mhuri wa baraza hilo pamoja na sahihi ya Rais wa TEC, Wolfgang Pisa pamoja na Katibu Mkuu, Padri Dk Charles Kitima likiwa na kichwa kinachosomeka ‘TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA (TEC) KUHUSU AMANI KWA TAIFA KUELEKEA SIKU YA UCHAGUZI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA UTAKAOFANYIKA TAREHE 29 OKTOBA 2025’.
Chapisho hilo ambalo pia liliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari bila kuhakikiwa, limepokelewa kwa sura na mitazamo tofauti na baadhi ya wadau na kuzua mijadala katika mitandao ya kijamii kutokana na ajenda yake inayogusa moja kwa moja Uchaguzi Mkuu 2025.
Ukweli ni huu
TEC imekanusha waraka huo na kusema ni batili na haujatolewa na baraza bali umetengenezwa na wapotoshaji kwa lengo la kupotosha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Padri Dk Kitima imeeleza kuwa TEC haihusiki na maudhui yeyote yaliyopo kwenye waraka huo feki na kusisitiza waumini na watanzania kuupuuza.
“Tunapenda kuwatangazia waumini na watanzania wote kwa ujumla, kuwa waraka huo haukutolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,” imeeleza taarifa ya TEC
Aidha, TEC imeonya vikali na kuwataka wapotoshaji na wote wenye tabia ya kughushi taarifa kama hizo kukoma mara moja.
“Tabia hii mbaya ya kutumia Taasisi ya Maaskofu kupitisha jumbe zisizotokana na baraza ikomeshwe” imesisitiza TEC.
Latest



