Si kweli: Mohammed Dewji amezindua sarafu mpya ya kidijitali Tanzania
- Asema akaunti yake ya X imedukuliwa akiwataka Watanzania kupuuzia ujumbe huo.
Dar es Salaam. Huenda umekutana na taarifa inayobainisha kuwa Bilionea na mfanyabiashara, Mohammed Dewji amezindua sarafu mpya ya kidijitali iitwayo Tanzania Coin ($Tanzania), habari hiyo si ya kweli na unapaswa kuipuuza.
Taarifa hiyo ilichapishwa na kusambaa kupitia akaunti yake ya mtandao wa X zamani Twitter jana Februari 5, 2025 ambapo sehemu ya chapisho hilo lilisomeka “Nataka kuifanya Tanzania kuwa rejea ya kupitishwa kwa cryptocurrency, kama vile @nayibbukele alivyofanya kwa El Salvador.”
Ujumbe huo ulifuatwa na chapisho jingine likisema, “Ni heshima kuwaletea watu ubunifu huu. Mustakabali wa fedha za kidijitali unaanza hapa.”

Chapisho hilo lilifuatana na kiungo cha tovuti kinachodai kuelekeza watu kwenye maelezo ya jinsi ya kuwekeza kwenye sarafu hiyo na baadae ilichapishwa video ya mtu anayefanana na Mohamed Dewji akithibitisha kuwa akaunti yake haijaibiwa na yaya ndiye aliyeanzisha sarafu hiyo.
Watu wengi walipokea taarifa hizo kwa shauku, huku wengine wakihoji uhalali wake kupitia sehemu ya maoni na baadhi ya vyombo vya habari viliripoti tukio hilo kwa uzito wake kabla ya baadae kubainika ni jaribio la ulaghai.
Ukweli ni huu
Wakati Nukta Fakti ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa taarifa hiyo saa mbili baadae kupitia akauti yake ya Instagram Mohammed Dewji alikanusha vikali taarifa hizo na kufichua kuwa akaunti yake ya X imedukuliwa.
Katika ujumbe wake aliandika, “Akaunti yangu ya X imevamiwa. Tafadhali puuzia posti zozote au meseji zisizo za kawaida. Tunalifanyia kazi kwa haraka ili kurejesha usalama wa akaunti. Kaeni makini.”
Mpaka kufikia Februari 6, 2025, saa 3:00 asubuhi, akaunti yake ya X bado ilikuwa chini ya wadukuzi, wakiendelea kuchapisha ujumbe wa uongo na kutuma viungo vya tovuti na makundi ya Telegram yanayodai kutoa maelekezo ya uwekezaji kwenye Tanzania Coin.
Nukta Fakti inathibitisha kuwa taarifa za Mohammed Dewji kuzindua Tanzania Coin si za kweli. Ni jaribio la ulaghai mtandaoni linalolenga kuwadanganya watu wawekeze pesa zao kwenye mpango usio rasmi.
Pamoja na kwamba viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa matamko ya kuanzisha mifumo ya kusimamia sarafu za kidijitali bado haijatangazwa rasmi lini Tanzania itatambua na kuruhusu matumizi ya sarafu za kidijitali.
Viashiria vingine vya udanganyifu vilivyopo kwenye taarifa hiyo ni hakuna tangazo lolote rasmi kutoka kwa Mohammed Dewji kupitia vyanzo vyake halali kama tovuti yake, kampuni zake au vyombo vya habari kuhusu uwepo wa sarafu hiyo.
Aidha machapisho hayo yana makosa ya kisarufi na uandishi jambo ambalo si la kawaida kwa ujumbe rasmi wa bilionea huyo.
Hata hivyo, kiungo cha tovuti kilichowekwa kwenye machapisho hayo hakina kikoa cha usalama cha Serikali (gov) au cha kampuni rasmi, dalili ya kuwa ni jaribio la ulaghai mtandaoni.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini pia kuwa video inayomuonesha mtu anayefanana na Dewji kuwathibitishia watu kuhusu urasmi wa sarafu hiyo ni ya kutengenezwa kwa kutumia akili unde (AI) na si halisi.
Wananchi wanashauriwa kuwa waangalifu na kuhakikisha wanapata taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika kabla ya kuwekeza katika miradi yoyote ya fedha za kidijitali.
Pia, ni muhimu kuripoti akaunti yoyote inayotilia shaka kwa mamlaka husika ili kusaidia kudhibiti uhalifu wa mtandaoni.
Kwasasa Mo Dewji amefanikisha kuirejesha akaunti yake ya mtandao wa X kwenye udhubiti wake na maeomba radhi kwa kufanya chapisho linalosomeka “Tunaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na uvamizi wa akaunti yangu. Tumesha dhibiti hali, lakini tunawasihi kuwa makini na ulaghai na kuhakikisha mnapata taarifa sahihi kutoka vyanzo vyetu rasmi,” ameandika Mo Dewji.

Latest



