Si kweli: Mkuu wa Mkoa wa Arusha amewachapa viboko wakandarasi
- Aliwachapa wanafunzi na wafanyabiashara walionunua viti vya shule na kuviuza kama chuma chakavu.
Dar es salaam. Kumekuwa na taarifa ambazo zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii hususan katika Mtandao wa X ( zamani Twitter) zinazodai Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi amewachapa fimbo wakandarasi kwa kosa la kuchelewesha samani za shule, taarifa hiyo si ya kweli.
Moja kati ya taarifa hizo imesambazwa na akaunti yenye jina ‘The Nairobi Times’ ambayo imechapisha taarifa inayosomeka “Taharuki Tanzania: Mkuu wa Mkoa wa Arusha anaswa kwenye video akipiga viboko wakandarasi kwa kuchelewesha samani za shule”.
Katika hatua nyingine, akunti yenye jina la Dr. Miguna Miguna imechapisha maudhui sawa na yale yaliypchapishwa na ‘The Nairobi Times’ yakiwa na ujumbe unaosomeka “Waafrika wanapaswa kupinga na kukomesha aina hizi za ukatili unaofanywa na wenye madaraka.
“Huyu ni Mkuu wa Mkoa wa Tanzania akiwashambulia wakandarasi kwa mikono yake mwenyewe. Ni kitendo cha aibu na cha kulaumiwa kupita kiasi”.

Aidha, chaneli mbalimbali za mtandao wa Youtube pia zimetumia video hiyo, ikiwemo chaneli ya GC News Hub ambayo imechapisha video hiyo kwa kichwa cha habari cha habari kinachosomeka ““Taharuki! wakandarasi wapigwa kama watoto kwa kushindwa kuwasilisha samani shuleni Tanzania”
Nukta Fakti imefanya uchunguzi na kubaini taarifa hiyo si ya kweli na picha iliyotumika kusambaza taarifa hiyo imetumika katika muktadha tofauti ili kupotosha.
Ukweli ni Huu
Tukio linaloonekana kwenye video ni la kweli na linamshusisha Kihongosi ambaye kwa sasa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Arusha ingawa tukio hilo lililotokea Disemba 17, 2020 wakati Kihongosi kiwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Siku hiyo, Kihongosi aliwaadhibu kwa viboko wanafunzi walioiba na wafanyabiashara walionunua viti vya shule kama chuma chakavu.
Hivyo video na picha zimetumika katika muktadha tofauti ili kupotosha.
Taarifa hiyo iliripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Bongofive na Global Tv ambavyo vyote vinaonesha tukio hilo ni la mwaka 2020.
Latest



