Si kweli: Maganda ya ndizi yanang’arisha meno

August 10, 2024 1:44 pm · Mlelwa Kiwale
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu wa afya wamefafanua kuwa ndizi hazing’arishi meno.
  • Ung’arishaji meno hufanywa katika kliniki maalumu za meno au hospitali.

Huenda umewahi kukutana na taarifa nyingi kuhusiana na njia mbalimbali za kung’arisha meno au kuyafanya yawe meupe kwa kutumia viungo, chakula au matunda.

Kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika kuwa maganda ya ndizi yanaweza kusaidia kung’arisha meno ambapo wasambazaji wa taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii hususan Tiktok na Youtube  ambapo katika moja ya video muandaaji anasikika akisema maganda ya ndizi husaidia kuponya magonjwa ya fizi na hung’arisha meno jambo ambalo si kweli.  

Ukweli huu hapa

Nukta Fakti imezungumza na madaktari pamoja na wataalamu wa kinywa ambao wamethibitisha kuwa jambo hilo kuwa ni uvumi wakisisitiza matumizi ya maganda ya ndizi hayana mahusiano ya moja kwa moja kung’arisha meno au kuyafanya yawe meupe.

Dk Alexander Haule ambaye ni mtaalamu wa meno kutoka Hospitali ya Taifa Mhimbili ameiambia Nukta Fakti kuwa matokeo ya maganda ya ndizi kwenye kung’arisha meno ni madogo kulinganisha na linavyotajwa na kuhamasishwa. 

“Hakuna kitu kama hicho kwamba maganda ya ndizi kufanya meno kuwa meupe bali effect (matokeo) yake ni madogo sana ukitumia hiyo, ni bora ufanye teeth whitening(kusafisha meno kitaalam) tu kama unataka meno meupe”, amebainisha daktari Alexander Haule kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Aidha tovuti ya masuala ya afya ya nchini Marekani iliyoandikwa na daktari wa meno Gerry Curatola ya Gonorado imebainisha kuwa kulingana na tafiti za kisayansi matumizi ya maganda ya ndizi hayafanyi meno kuwa meupe.

“Kwa hiyo maganda ya ndizi hufanya tu kuondosha ule unjano uliopo katika meno na sio kufanya meno kuwa meupe,” imebainisha tovuti hiyo.

Tovuti hiyo imeongeza kuwa si tu maganda ya ndizi bali matumizi ya vitu vingine kama baking soda, mkaa, mafuta pamoja na vinega kama mbinu ya kung’arisha meno haina matokeo chanya.

Wataalamu wa afya wamefafanua kuwa matumizi sahihi ya ung’arishaji meno ni kwa kutumia njia husika zilizopitishwa katika vituo vya afya au wataalamu wa afya na sio kutumia njia za kienyeji  kama maganda ya ndizi.

Daktari Bernard Kairuki kutoka hospitali ya Ndovu iliyopo jijini Dar es Salaam ameshauri wananchi kujenga utaratibu wa kutembelea madaktari angalau mara mbili kwa mwaka ili kulinda afya ya meno na kinywa mbali na utaratibu wa kawaida wa kupiga mswaki kila siku.

Enable Notifications OK No thanks