Shule za msingi, sekondari zafungwa kujikinga na Corona Tanzania

March 17, 2020 1:23 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Zimefungwa kwa siku 30 na wanafunzi watakiwa kubaki nyumbani.
  •  Mikusanyiko yote ya ndani na nje isiyokuwa ya lazima ikiwemo mikutano ya kisiasa imepigwa marufuku.
  • Wafanyabiashara wanaolangua vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kudhibiti maambukizi (hand sanitizer) waonywa. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kufungwa kwa shule zote za awali, msingi na sekondari kwa siku 30, kusitisha mikutano ya kisiasa na michezo yote inayohusisha makundi ya watu nchini Tanzania ili kujikinga na kusambaa kwa virusi vya Corona. 

Tanzania imekuwa nchi ya tatu Afrika Mashari baada ya Kenya na Rwanda kuthibitisha kuwepo kwa mgonjwa mmoja wa virusi vya Corona huku takwimu za Shirika za Afya Ulimwenguni (WHO) za jana (Machi 16, 2020) zinaeleza kuwa watu 167,511 wameambukizwa ugonjwa huo duniani huku waliofariki wakifikia 6,606.

Majaliwa akitangaza tamko maalum la Serikali kuhusu ugonjwa wa Corona leo (Machi 17, 2020) amesema Serikali imesitisha mikusanyiko yote ya ndani na nje isiyokuwa ya lazima kuanzia sasa ikiwepo ya semina, warsha, makongamano, matamasha ya muziki na mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa. 

Ameagiza shule zote za msingi na sekondari zifungwe kwa siku 30 kuanzia leo na wanafunzi warejee nyumbani ili kuwaepusha na hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi duniani.

“Lakini pia tumefunga shule zote za awali, shule za msingi, shule za sekondari na kidato cha sita na zitafungwa kwa muda wa siku 30 inaanzia tarehe hii ya leo ya Machi 17. 

“Na wizara itafanya marekebisho ya mitihani ya kidato cha sita ambao wanatarajia kufanya mitihani Mei 4 watakuwa na muda mfupi kwa hiyo itasogezwa mbele kadiri ya matokeo yatakavyojitokeza ili wapate muda wa kusoma,” amesema Majaliwa. 

Aidha, amesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama vile Ligi Kuu ya Tanzania bara, ligi daraja la pili, Ligi daraja la kwanza lakini pia michezo ya shule za msingi (UMITASHUNTA), michezo ya shule za sekondari (UMISETA) pamoja na ile ya mashirika ya umma. 

“Kwa hiyo michezo yote hiyo imesitishwa kwa kipindi cha mwezi mmoja,” amesema Majaliwa na kuagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuyataarifu mashirikisho yote ya michezo kuhusu mabadiliko hayo ya ratiba. 


Zinazohusiana


Awataka Watanzania kuchukua tahadhari

Waziri Mkuu amesema licha ya hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Serikali itaimarisha ukaguzi na ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili kuwabaini wasafiri wenye dalili za ugonjwa na viashiria vyenye hatari.

Serikali inaendelea kuwajengea uwezo (mafunzo) watumishi wa sekta ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo jinsi ya kutoa tiba, kuchukua sampuli, uelimishaji na kuzingatia kanuni za afya.

“Serikali imetenga hospitali maalum za Mloganzila (DSM), Kituo cha Buswelu (Mwanza) na Hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja (Zanzibar) na Chake Chake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika,” amesema Majaliwa. 

Ameiagiza Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kudhibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na kuongeza kwamba Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa vifaa hivyo.

Amewataka Watanzania wazingatie ushauri unaotolewa na Serikali na kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii. 

“Watanzania tuache mzaha wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa tahadhari katika jambo hili,” amesisitiza Majaliwa. 

Enable Notifications OK No thanks