Shule za msingi, sekondari kufunguliwa Juni 29

June 16, 2020 1:33 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kupungua kwa ugonjwa wa virusi vya Corona Tanzania. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza kufunguliwa kwa shule zote za awali, msingi na sekondari ifikapo Juni 29 mwaka huu zilizokuwa zimefungwa kwa miezi mitatu kutokana na janga la virusi vya Corona kwa sababu ugonjwa huo umepungua kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania. 

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Juni 16, 2020) jijini Dodoma wakati akifunga Bunge la 11, amesema maisha na shughuli zingine ikiwemo masomo lazima yaendelee kama kawaida. 

“Kutokana na hali ya ugonjwa wa Corona kuendelea vizuri na kwa kweli imepungua sana. Napenda nitumie nafasi kutangaza kwamba kuanzia tarehe 29 nafikiri itakuwa Jumatatu mwezi huu wa Juni shule zote zifunguliwe zilizokuwa zimebaki,” amesema Dk Magufuli.

Serikali ilifunga shule na vyuo vyote nchini Machi mwaka huu ili kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo wa COVID-19. 

Juni mosi, Rais aliruhusu vyuo vyote kufunguliwa na wanafunzi wa kidato cha sita kurejea shuleni ili kujiandaa na mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari.  

“Maisha lazima yarudi kama ilivyokuwa zamani. Hata hivyo, naendelea kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na pia kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wetu wa afya kwasababu ni muhimu kuzingatia hilo,” amesema Rais Magufuli wakati akiagiza kufunguliwa kwa shughuli zote zilizokuwa zimezuiliwa ikiwemo ndoa. 


Zinazohusiana:


Aidha, amesema siyo tu Tanzania imefanikiwa kuushinda ugonjwa huo lakini pia kupunguza athari zake zikiwemo athari za kiuchumi.

“Kama mnavyofahamu Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF)yamebashiri kwamba asilimia 60 ya nchi za Afrika zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara zitashuhudia ukuaji hasi yaani negative wa uchumi Mwaka 2020. 

Hata hivyo, sisi Tanzania kutokana na hatua tulizozichukua, uchumi wetu hautokua kwa negative. Utaendelea kukua vizuri angalau kwa asilimia 5.5 au zaidi,” amesema.

Enable Notifications OK No thanks