Shule 10 bora matokeo kidato cha sita 2022
- Shule ya Sekondari Kemebos ya mkoani Arusha ikishika nafasi ya kwanza kitaifa.
- Tabora yaongoza kuingiza shule nyingi.
- Feza Boys na Kibaha Boys zakimbizwa 10 bora.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2022 huku Shule ya Sekondari Kemebos ya mkoani Kagera ikishika nafasi ya kwanza kitaifa.
Akitangaza matokeo hayo leo Julai 5, 2022 Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amas amesema Kemebos imeungana na shule nyingie tisa katika 10 bora ya kitaifa ambazo zimefanya vizuri.
Kemebos haikuwepo katika 10 ya mwaka jana lakini imepambana na kuitoa Kisimiri ya mkoani katika nafasi ya kwanza na kuishusha nafasi ya pili mwaka huu.
Kisimiri imefuatiwa na Tabora Boys ya mkoani Tabora katika nafasi ya tatu, Tabora Girls (Tabora) imeshika nafasi ya nne huku Ahmes ya Pwani ikifunga tano bora kitaifa.
Nafasi ya sita imeenda kwa Shule ya Sekondari ya Dareda ya mkoani Manyara, Nyaishozi (Kagera), Mzumbe (Morogoro), Mkindi (Tanga) huku Ziba ya Tabora ikifunga orodha ya shule 10 bora kitaifa.
Tabora inaongoza kuingiza shule nyingi katika orodha hiyo ya dhahabu ambapo imeingiza shule tatu ikifuatiwa na Kagera yenye shule mbili. Mikoa iliyobaki imetoa shule moja moja.
Soma zaidi:
-
Matokeo kidato cha sita 2022 yatangazwa, ufaulu waongezeka kidogo
- Matokeo kidato cha sita 2022 haya hapa
Mchuano mkali
Matokeo ya mwaka huu yaliyotangazwa visiwani Zanzibar yameshuhudia shule ya tatu mpya zikiingia 10 bora kitaifa ambazo hazikuwepo mwaka jana. Shule hizo ni Mkindi, Nyaishozi na Ziba.
Shule maarufu kama Feza Boys ya mkoani Pwani, Kibaha Boys (Pwani) na Ilboru ya Arusha zimetupwa nje kwenye 10 bora ya mwaka huu ambapo shule ya Feza Boys imeshika nafasi ya 29 kitaifa na ya tatu kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Mwaka 2021, Feza Boys ilishika nafasi ya sita kitaifa.
Shule ya Kibaha, ufaulu wake katika mpangilio wa shule umeendelea kushuka tangu mwaka 2019, jambo linaloacha maswali mengi kuhusu shule hiyo kongwe Tanzania.
Mwaka 2019 ilishika nafasi ya pili kitaifa lakini mwaka uliofuata ikaporomoka hadi nafasi ya nane kabla haijashika nafasiu ya 20 mwaka jana.
Mwaka huu imeshika nafasi ya 33 kitaifa.
Aidha Amasi amesema jumla ya watahiniwa wa kidato cha sita 95,826 walisajiliwa kufanya mtihani huo Mei mwaka 2022 ambapo wasichana walikuwa 41,517 sawa na asilimia 43.33.
Kati yao, watahiniwa 94,456 sawa na asilimia 98.57 walifanya mtihani na watahiniwa 1370 sawa na 1.43 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.
Latest



