Shughulikieni changamoto zinazorudisha nyuma haki za binadamu

December 8, 2022 1:55 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Changamoto hizo ni pamoja na mauaji ya wanawake na ukatili wa kijinsia.
  • Licha ya changamoto hizo utekelezaji wa haki za binadamu nchini unaongezeka.

Dar es Salaam. Serikali imesema utekelezaji wa haki za binadamu ikiwemo uhuru wa watu kujieleza unazidi kuimarika Tanzania huku wadau wakitaka changamoto zinazorudisha nyuma haki hizo zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu.

Mkurugenzi wa haki za binadamu Wizara ya Katiba na Sheria, Ngasory Sarakikya aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya haki za binadamu  yaliyofanyika leo (Disemba 8, 2022) jijini Dar es Salaam amesema moja ya haki hizo zinazoimarika ni haki za kisiasa na demokrasia.

“Haki za kisiasa na demokrasia nchini zimekuwa zikiimarika kutokana na Serikali kukutana na kufanya majadiliano ya vyama vyote vya siasa na wadau,” amesema Sarakikya aliyekuwa akimuwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro.

Hayo yamejiri ikiwa ni miezi 11 tangu kuundwa kwa kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia na vyama vya siasa kilichoundwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Oktoba 21, 2022 kikosi kazi hicho kiliwasilisha maoni 18 yenye lengo la kukuza demokrasia chini.

Mbali na haki za kisiasa haki nyingine zilizoripitwa kuimarika ni pamoja na haki za kiuchumi, kiraia, elimu na kupata huduma za kijamii ikiwemo maji.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ili wananchi waendelee na kunufaika na uhuru wa kutoa maoni na haki ya kutoa na kupata taarifa,” amesema mwakilishi huyo wa waziri.

Licha ya haki za binadamu kuimarika nchini, bado wadau wa masuala ya utawala na sheria wanasisitiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika kuwawezesha Watanzania kunufaika na haki hizo kwa sababu hawazipati kwa kiwango kinachohitajika. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Wakili Anna Henga  ametaja changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi inayovunjwa kutokana na mauaji ya watu yanayoendelea nchini.

“Bado kuna changamoto mbalimbali, kwa mfano haki ya kuishi, haki ya kuwa huru na salama vinaendelea kuwa changamoto,” amesema Wakili Henga.

Mbali na matukio hayo ameainisha matukio mengi ikiwemo mauaji yanayofanywa na  vikundi vya uhalifu kama panya road, Mauaji ya wenza yanayosababishwa na mume au mke  pamoja na kujiua.


Soma zaidi


“Kuanzia Januari mpaka Disemba mwaka 2022 matukio 37 ya mauaji ya wenza  yaliripotiwa, sababu kubwa ikiwa wivu wa mapenzi,”” ameongeza mkurugenzi huyo.

Naye Patient Ntwina, Katibu Mtendaji wa Tume ya Hazi za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) amesema ingawa haki hizo zinazidi kuimarikani ni vyema Serikali kuchukua hatua juu ya changamoto zinazorudisha nyuma jitihada hizo kwani kila binadamu ana haki ya kuishi.

“Binadamu wote tunastahili kutendewa haki, kwa utu na kwa heshima na sisi sote tulizaliwa sawa na tunapaswa kutendewa kwa usawa,” amesema Ntwina.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta-Ozaki Macias amesema tafiti zinaonyesha kwamba jamii za kidemokrasia, shirikishi na zenye usawa zinatoa fursa kwa kila mtu kufanikiwa na kujitengenezea mustakabali mwema wanaostahili.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW