Shabiki wa Taifa Stars ateuliwa balozi wa utalii Uingereza

February 5, 2020 4:25 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Meneja Masoko kutoka Bodi ya Utalii (TTB), Geofrey Meena(kushoto) akimkabidhi barua ya utambuzi  balozi wa hiari wa utalii wa Tanzania nchini Uingereza, Nick Reynald ‘Bongozozo’(katikati)  aliyekabishiwa barua hiyo katika Ofisi za TTB Dar es Salaam,  leo Februari 04,2020. Kulia ni Afisa Uhisiano Mkuu wa TTB, Geofrey Tengeneza.


  • Ni rais wa Uingereza, Nick Reynald a.k.a Bongozozo.
  • Ameishi Tanzania kwa miaka 18 na ni shabiki mkubwa wa timu ya Taifa ya Taifa Stars.
  • Atasaidia kuvutia watalii kutoka Uingereza kupitia mitandao yake ya kijamii.

Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), imemteua shabiki wa timu ya Taifa Stars, Nick Reynald a.k.a Bongozozo kuwa balozi wa hiari wa utalii nchini Uingereza ili kuongeza idadi ya watalii wanaotoka katika nchi hiyo ya Ulaya.  

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kingwalla alilolitoa Jijini Dodoma Februari 3, 2020 la kumpa Mwingireza Bongozozo ubalozi wa utalii wa Tanzania nchini Uingireza.

Akizungumza katika hafla ya kumkabidhi barua ya utambuzi kwa ajili ya kazi hiyo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa TTB, Geofrey Meena amesema kuwa, Reynald aliyezaliwa Zimbabwe na kuishi Tanzania kwa miaka 18 atakuwa balozi mzuri kwa utalii wa Tanzania kwa sababu maeneo mengi ya utalii anayajua.

“Bodi inayo furaha leo kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana ya Utalii nchini, kumkabidhi rasmi Nick Reynald ‘Bongozozo’ barua ya uteuzi wa kuwa balozi wa hiari wa  utalii wa Tanzania nchini Uingereza kama kituo bora cha utalii Afrika na duniani kote,” amesema Meena.

Meena amesema kuwa Bongozozo alivutiwa sana na soka la Tanzania kwa kuwa kuna fujo isiyoumiza na amekuwa akisafiri na Taifa Stars katika michuano mbalimbali ikiwemo ile ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo kwa mwaka 2019 ilifanyika nchini Misri.

“Amekuwa maarufu sana hapa nchini kutokana na  mapenzi makubwa kwa Tanzania ambayo yemejidhihirisha katika nyanja nyingi ikiwemo ushabiki wa mpira kwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars” pamoja na wachezaji akiwemo Mbwana Samatta anayecheza klabu ya mpira ya Astoni villa nchini Uingireza,” amesema Meena.


Soma zaidi: 


TTB imedhamiria kukuza utalii kwa kuongeza watalii kutoka Uingereza kwa kuwa nchi hiyo ni ya pili kwa kuleta watalii wengi nchini ikitanguliwa na Marekani, 

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, takwimu zinaonyesha watalii kutoka Uingereza waliotembelea Tanzania mwaka 2018 walikuwa 77,199 huku Marekani ikileta watalii 94,876.

Kwa upande wake, Bongozozo  amesema kuwa yeye atakuwa balozi mzuri katika kutangaza mazuri ya Tanzania na utalii wake duniani kote kupitia mitandao yake ya kijamii ili kuleta watalii nchini.

“Nikizunguka duniani kote kupitia mitandao yangu ya kijamii nitawaambia kuwa Tanzania ni nchi yenye watu wakarimu sana, nitazidi kuipeperusha bendera ya Tanzania na nitawaeleza sehemu za kitalii zilizoko Tanzania.

“Kwahiyo nimekubali kuitangaza Tanzania kwa watalii wengi duniani”, amesema ‘Bongozozo.

Enable Notifications OK No thanks