Serikali yatoa ufafanuzi tuhuma za rushwa muuguzi wa afya Kigoma

September 2, 2025 6:49 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Chanzo cha taharuki iliyotokea ni mtego uliowekwa na uongozi wa hospitali kumkamata muuguzi aliyedaiwa kuomba rushwa.

Dar es Salaam. Serikali imesema vyombo vya usalama vinachunguza tuhuma za rushwa zinazomkabili muuguzi wa afya wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo iliyopo mkoani Kigoma.

Taarifa hiyo ya Serikali imekuja kufuatia taharuki iliyotokea mara baada ya video iliyomuonesha muuguzi wa afya akilalamika kuondolewa wodi ya wanawake waliojifungua na askari kwa nguvu wakati akitoa matibabu kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Video hiyo ilianza kusambaa usiku wa kuamkia Agosti 31, ikimuonesha mhudumu wa afya akilalamika kuvamiwa na kuondolewa ghafla bila kujua kosa lake, huku akidai alikuwa akimsaidia mjamzito kujifungua na kutoa kondo la nyuma la uzazi.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Septemba 2, amesema si kweli kuwa muuguzi huyo alikuwa akimtoa mgonjwa kondo la nyuma la uzazi kwa kuwa mgonjwa alijifungua kwa njia ya oparesheni na kondo huondolewa baada tu ya kujifungua.

Aidha, Dk Magembe  amesema wodi aliyokuwepo muuguzi huyo ni maalumu kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya wagonjwa waliojifungua kwa oparesheni akiongeza kuwa purukushani zilizotokea zilizotaka na muuguzi huyo kuhusishwa na tuhuma za rushwa ambapo siku ya tukio aliwekewa mtego.

“Zipo taarifa kwamba mtumishi huyo amekuwa na tabia ya kuomba rushwa, wasamalia wema walitoa taarifa kuwa mama yule (mgonjwa) ameombwa Sh 60,000 na mtumishi ili afanyiwe upasuaji, na yule mama na familia yake walitoa Sh39,000…

Kilichofanyika ni hospitali kuweka mtego, ili wakati yule mama anamalizia Sh 21,000 waweze kumkamata yule mtumishi na ndicho kilichonekana pale,” amesema Dk Magembe.

Kwa mujibu wa Dk Magembe mabishano kati ya askari aliyetumwa kumkamata muuguzi na muuguzi mwenyewe ndiyo yaliyozua taharuki kwenye jamii.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali amesema zipo hatua zitakazochukuliwa na vyombo vya usalama pamoja na mabaraza ya kitaaluma iwapo tuhuma za muuguzi huyo zitathibitika kuwa ni za kweli ambapo kwa sasa tayari ameshasimamishwa kazi.

“Suala hili kwa sasa limekabidhiwa kwa vyombo vinavyohusika na uchunguzi ili kujua kama ni kweli, kwa sasa tusubiri uchunguzi uishe kisha taarifa itatoka,” amesema Dk Magembe.

Hii si mara ya kwanza kwa wauguzi nchini Tanzania kukabiliana na tuhuma za uvunjifu wa maadili na miiko ya kazi zao ambapo mwaka 2023 wauguzi wawili walifukuzwa kazi baada ya kusababisha kifo cha mjamzito kwa kukataa kumpa huduma anazostahili.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW