Serikali yatoa onyo uchaguzi Serikali za Mitaa
- Yawataka wadau watakaoshiriki uchaguzi huo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu zilizowekwa.
- Watakaokiuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
- Wananchi wahimizwa kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wanaowataka.
Dar es Salaam. Wadau watakaoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa amani kwani Serikali haitasita kuchukua hatua pale itakapothibitika vitendo hivyo kufanyika.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wadau hao mbalimbali kutoka vyama vya siasa, taasisi za Serikali, zisizo za Serikali na wananchi ni vema wakahakikisha wanasoma na kuelewa kanuni na miongozo ya uchaguzi huo ili waweze kushiriki ipasavyo.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Septemba 13, 2019) wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma, amewataka Watanzania wote wenye sifa washiriki uchaguzi huo kwani ni haki yao ya msingi.
Amewataka Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi huo wahakikishe wanazielewa kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze kutoa tafsiri sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo.
Mbali na wadau hao, pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu katika kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi kwenye mazingira ya amani na utulivu bila kubugudhiwa.
Soma zaidi:
- Majaliwa: Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache
- Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho.
- Majaliwa awataka vijana kujitokeza kwa wingi uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.
Uchaguzi huo unafanyika kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kukidhi matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inayoelekeza kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi.
Kuhusu uboreshaji wa daftari la wapiga kura, Waziri Mkuu amesema Julai 18, 2019 Serikali ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro na linaendelea vizuri katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kwa sasa zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba).
Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini ya kaulimbiu isemayo Kadi Yako, Kura Yako, Nenda Kajiandikishe.