Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho

November 21, 2018 9:07 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aagiza elimu ya upangaji madaraja ya korosho itolewe. Picha| Mwananchi.


  • Elimu hiyo itawahusu  maafisa ushirika, viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS), maafisa ugani na wakulima ili kuwawezesha kubaini na kupanga korosho katika madaraja kuanzia ngazi ya vyama vya msingi.
  • Amesema semina hiyo ifanyike mwakani ili maafisa ushirika baada ya kupata mafunzo wawasaidie wakulima kwenye msimu ujao watambue korosho walizopeleka kama zina ubora unaokubalika sokoni.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza warajisi wasaidizi wa ushirika katika mikoa yote inayolima korosho nchini waandae semina kwa maafisa ushirika, viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS), maafisa ugani na wakulima ili kuwawezesha kubaini na kupanga korosho katika madaraja kuanzia ngazi ya vyama vya msingi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema jambo hilo litamsadia mkulima kujua korosho ina ubora gani kabla hajaipeleka soko ambapo inapofika katika ghala kuu wafanye kazi ya kuthibitisha ambapo hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kuhusu madaraja.

“Zoezi hili licha ya kuthibitisha ubora litasaidia kuboresha uzalishaji kwani wataelimishwa namna ya kuimarisha na kuboresha uzalishaji wa korosho nchini ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya viuatilifu,” amesema Majaliwa.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Novemba 21, 2018) wakati alipotembelea kiwanda cha korosho cha BUKO kilichopo katika manispaa ya LIndi ambapo ameshuhudia korosho zikipimwa ubora kwenye ghala kuu lililopo kiwandani hapo.


Zinazohusiana:


Amesema semina hiyo ifanyike mwakani ili maafisa ushirika baada ya kupata mafunzo wawasaidie wakulima kwenye msimu ujao watambue korosho walizopeleka kama zina ubora unaokubalika sokoni.

Katika semina hiyo watakutanishwa maafisa kilimo na maafisa ushirika ili wapate taaluma hiyo itakayowawezesha kupima korosho na kuitenga katika madaraja na kuwaondolewa usumbufu wakati wa mauzo.

Mrajisi Msaidizi wa ushirika mkoa wa Lindi, Robert Nsunza amemuhakikishia Majaliwa kuwa wataandaa semina hiyo kwa wahusika ili kuwasaidia wakulima kutambua madaraja ya korosho zao kuanzia ngazi ya kijiji.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Nangomba Holdings, Ramadhani Katau ambaye ndiye mtunzaji wa ghala la korosho katika kiwanda cha BUKO, amesema ghla hilo lina uwezo wa kupokea na kutunza tani 10,000 za korosho ambapo hadi sasa tani zilizopo ghalani ni 6,370.

Ukusanyaji wa korosho unaofanywa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) unaendelea kwa sasa, baada ya Serikali kuzipiga kampuni binafsi kununua korosho ya wakulima kutokana na utata wa bei uliojitokeza katika msimu wa mwaka hu. 

Enable Notifications OK No thanks