Serikali yamuhoji Nabii aliyedai kugundua dawa ya kutibu virusi vya Corona
- Imesema inataka athibitishe madai yake ya kuwa ana dawa ya kutibu ugonjwa huo.
- Imesema akishindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua kali za kisheria.
- Mpaka sasa, Serikali imesema hakuna mgonjwa yeyote aliyegundulika kuwa na virusi hivyo nchini.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inamuhoji mkazi wa mkoa wa Arusha, Mosses Mollel anayejiita Nabii namba saba ili athibitishe madai yake kuwa ana uwezo wa kutibu virusi vya ugonjwa wa #Corona ambavyo mpaka sasa vimeua watu zaidi ya 1,300 ulimwenguni.
Hata hivyo, imewahakikishia Watanzania kuwa nchi bado iko salama na hakuna mgonjwa yeyote aliyeambukizwa virusi hivyo.
“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu anayejiita Nabii Saba kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa wa Corona, ila hapa kwetu Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huyo, tunachotaka huyo mtu atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa wa Corona,” amesema Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile jana (Februari 13, 2020) mkoani Arusha.
Amesema hadi sasa Serikali imetuma wataalamu wake kwenda kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali vya kutoa huduma ya tiba na kujitangaza kuwa anatoa huduma ya kutibu ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa jumuiya za kimataifa zinahaha kusaka tiba ya ugonjwa huo.
“Tuepuke kutoa kauli ambazo zinakwenda kuchanganya jamii na endapo tutabaini mtu huyu hana sifa ambazo anasema kuwa nazo tutamchukulia hatua za kisheria,” amesema Dk Ndugulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Soma zaidi:
- Watanzania waishio China watolewa hofu virusi vya corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
Nabii Namba Saba ambaye ni mkazi wa Ngaramtoni Wilayani Arumeru mkoani Arusha amekuwa akijitangaza kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa huo wa virusi vya Corona na kuweka mawasiliano yake kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo YouTube .
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mlipuko huo hadi Februari 13 ulikuwa umewaambikiza watu 46 997 kote duniani na kuwauwa zaidi ya 1,368 ambapo asilimia 99 ya visa vya ugonjwa huo vimetokea China.
WHO kwa kushirikiana na wataalam wanaendelea na juhudi mbalimbali za kutafuta dawa ya ugonjwa huo ambao unasambaa kwa njia ya hewa na kushikana mikono na mgonjwa aliyeathirika.