Serikali yajibu madai ya ndege za Tanzania kuzuiwa anga la EU
- Tanzania inasubiri EU kukamilisha tathmini yake ili kubaini iwapo hatua zilizochukuliwa zinatosheleza kuondoa vikwazo hivyo.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa Umoja wa Ulaya (EU), ili kuyaondoa mashirika yake ya ndege katika orodha ya Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EU Air Safety List) iliyotolewa na umoja huo.
Hayo yamejiri wakati makumi ya vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa kuripoti taarifa ya EU ya kuzuia mashirika 154 ya ndege kutoka katika nchi 16 kutua katika anga la umoja huo kutokana na kutokukidhi vigezo vya kiusalama.
Hata hivyo, taarifa hiyo si mpya, ilichapishwa katika toleo la 48 la Usalama wa Anga la EU na kuchapishwa katika tovuti rasmi ya umoja huo Juni 9, 2026.
Serikali yajibu
Akijibu madai hayo Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema tayari wakaguzi kutoka EU walitembelea Tanzania Septemba, 2026 ili kufanya tathmini, huku wataalamu hao wakitambua hatua zilizopigwa wakati wa ziara yao nchini.
Hadi sasa, Tanzania inasubiri EU kukamilisha tathmini yake ili kubaini iwapo hatua zilizochukuliwa zinatosheleza kuondoa vikwazo hivyo.
EU Air Safety List (ASL) ni orodha rasmi inayotolewa na Tume ya Ulaya ikibainisha mashirika ya ndege yasiyokidhi viwango vya kimataifa vya usalama wa anga na ambayo yamepigwa marufuku au kuwekewa masharti ya kufanya safari katika anga la nchi wanachama wa umoja huo.Â

Orodha hiyo iliyoanzishwa mwaka 2006 pia inalenga kutoa tahadhari kwa abiria kuhusu mashirika yenye changamoto za usalama, hata kama hayafanyi safari kwenda Ulaya. .
Hata hivyo, vikwazo vilivyowekwa vinahusu nchi ambazo mamlaka zake za usafiri wa anga zimeonekana kuwa na mapungufu katika kutekeleza wajibu wa kusimamia usalama wa mashirika ya ndege yaliyosajiliwa chini yake.
Wasiwasi huo unahusisha upungufu wa wataalamu wenye sifa za kiufundi pamoja na udhaifu katika ufuatiliaji wa shughuli za safari za ndege na ubora wa kiufundi wa ndege (airworthiness).
Licha ya kuingizwa kwa mashirika hayo kwenye orodha hiyo haimaanishi kuwa kila moja limebainika kuwa na kasoro za kiusalama katika ukaguzi wake binafsi, bali vikwazo hivyo vinahusishwa na mapungufu katika mfumo wa usimamizi wa usalama wa anga nchini.
Mpaka sasa, Umoja wa Ulaya umeweka vikwazo vya usalama wa anga kwa nchi 12 za Afrika, huku ukizuia mashirika 87 ya ndege kutoka barani humo kufanya shughuli zake katika anga la nchi wanachama wake.
Kwa upande wa Tanzania, mashirika ya ndege 34, ikiwemo la Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Air Tanzania na Precision Air, yamejumuishwa kwenye orodha hiyo, ikiwa ndio idadi kubwa kuliko nchi nyingine yoyote kati ya nchi zilizoorodheshwa.Â
Aidha nchi nyingine za Afrika zilizopo katika orodha hiyo ni Angola, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Djibouti, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Liberia, Libya, Sao Tome na Principe, Sierra Leone, Sudan na Tanzania.