Serikali yaingilia kati ujenzi holela hifadhi ya Ziwa Manyara
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akivunja moja ya ukuta wa mwekezaji uliozuia wanyamapori kutoka nje ya eneo hilo, pembezoni mwa ziwa Manyara ilipo Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara katika Kijiji cha Migungani Wilaya ya Monduli. Picha| Wiziri ya Maliasili na Utalii.
- Yawapiga marufuku wawekezaji kujenga katika eneo hilo.
- Hiyo itawasaidia wanyamapori kuishi salama bila usumbufu.
Dar es Salaam. Serikali imeagiza wananchi na wawekezaji wanaoendelea kujenga katika eneo linalozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kuacha mara moja ili kuruhusu wanyama kuendelea kuishi katika ikolojia hiyo bila kubugudhiwa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo lililopo kwenye Kijiji cha Migungani B, wilayani Monduli katika Mkoa wa Arusha.
“Naelekeza uzio wote uliojengwa kuzunguka hili ziwa uvunjwe na mwekezaji yeyote tutakayemsikia anajenga uzio tutamchukulia hatua za kisheria,” amesisitiza Masanja.
Amesema kumekuwa na migogoro mingi kati ya wananchi na hifadhi baada ya kuvamia maeneo ya wanyama inayosababisha wananchi hao kuvamiwa na wanyama wakali kama tembo na kuwaasa wananchi kuchagua maeneo mazuri ya kuishi.
“Ifike mahali wananchi wahamie kwenye maeneo ambayo watakaa bila kubughudhiwa,” amesema Masanja.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Masanja amesema Serikali ina mpango wa kufanya tathmini ya mapito yote ya wanyama na wananchi wawe tayari kuyaachia ili kukuza utalii nchini Tanzania.
“Nakuelekeza Mkurugenzi fanyeni tathmini katika mapito yote ya wanyama ili kujua majengo na mali zote zilizopo ili tuwahamishe wananchi kwa kuwapa fidia ili wanyama hawa waweze kupita” amesisitiza Masanja.
Pia ameelekeza Maafisa Uhifadhi kufanya operesheni ya kuwatoa wanyama walio kwenye vizuizi vya kuta pembezoni mwa ziwa Manyara kabla ya mwisho wa mwaka huu ili wawe huru.
Ziwa Manyara limekuwa kivutio muhimu cha watalii kutokana na mandhari nzuri ya ziwa hilo yenye maua ya kuvutia na kupendeza.
Hata hivyo, muingliano wa wanyama na shughuli za binadamu umekuwa changamoto katika kuhifadhi eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisume amesema katika kikao cha awali kati yake na wahifadhi wamekubaliana wawe na kikao kila baada ya miezi mitatu ili kupitia maeneo yenye vibali vya ujenzi ili kutathmini kama eneo hilo ni ushoroba au la.
Amemtaka Diwani wa Kata ya Migungani Joseph Pareso kuwa na taarifa sahihi za watu wanaochukua ardhi katika eneo lake ili kuepusha migogoro inayojitokeza.
“Mheshimiwa Diwani lazima ajue nani amechukua ardhi, kiasi gani, maeneo gani na kwa sababu zipi,” amesema Mwaisume.
Latest
