Serikali yaanza uchunguzi ajali ya treni iliyoua watu watatu, kujeruhi 66 Dodoma

January 3, 2021 8:46 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Majeruhi wapelekwa Hospitali za Bahi na ya mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu

Dar es Salaam. Serikali imeanza uchunguzi wa chanzo cha ajali ya treni iliyotokea mkoani Dodoma jioni ya Januari 2 mwaka huu na kuua watu watatu na kuacha majeruhi 66.

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea kati ya Kigwe na Bahi ikiwa ni kilomita 58 tu kutoka Dodoma Mjini.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa mapema Jumapili Januari 3, 2021, Msemaji wa TRC Jamila Mbarouk amesema treni hiyo iliyokuwa na abiria 720 ilikuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na Mwanza.

“Mpaka sasa majeruhi ni 66 na waliopoteza maisha ni watu watatu akiwemo mtoto mmoja na watu wazima wawili,” amesema Mbarouk katika taarifa hiyo.

Msemaji huyo ameeleza kuwa majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali za Bahi na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

“Uchunguzi wa chanzo cha ajali unaendelea kufanyika na shirika litaendelea kutoa taarifa,” amesema Mbarouk.
Habari za ajali hiyo zilianza kusambaa jana kwenye mitandao ya kijamii huku akaunti ya Instagram ya Msemaji Mkuu wa Serikali ikithibitisha ajali hiyo na kueleza kuwa kulikuwa na “vifo vichache”.

Baadhi ya picha zilizokuwa zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii ukiwemo WhatsApp zilionyesha sehemu ya mabehewa yakiwa yamepinduka huku abiria walionusurika na ajali hiyo wakionekana kuwa katika taharuki.
Jamila amesema kuwa katika ajali hiyo, mabehewa sita kati ya 12 yalipata ajali.

Hii si mara ya kwanza kwa treni zinazofanya safari katika reli ya kati kupata ajali ndani ya miaka minne iliyopita. Miaka mitatu iliyopita Januari 2017 treni ya Delux iliyokuwa ikitokea Kigoma kwenda Dar es Salaam ilipata ajali katika eneo la Ruvu ambapo watu watano walijeruhiwa na hakuna aliyepoteza maisha. Pia, Juni 2019, treni ya TRC ilipata ajali karibu na Stesheni ya Dodoma na kujeruhi watu 32.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW