Serikali ya Tanzania kumuenzi bilionea Mufuruki kivitendo

December 11, 2019 12:31 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema itasikiliza maoni ya sekta binafsi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara.
  • Yasema inatambua mchango wake alioutoa katika kutengeneza ajira kwa Watanzania na kukuza uchumi.
  • Alifariki jumamosi nchini Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 60.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeahidi  kuendelea kumuenzi  mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki kwa kusikiliza maoni ya sekta binafsi yanayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. 

Mufuruki ambaye pia ni muhisani na kocha wa masuala ya uongozi, alifariki dunia siku ya Jumamosi (Desemba 7), nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki aliyekuwa akizungumza wakati wa kuaga mwili wa mfabiashara huyo katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), leo (Desemba 10, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema Serikali itamuenzi mfabiashara huyo aliyekuwa nguzo ya sekta binafsi kwa mawazo na vitendo. 

“Serikali tutaendelea kumuenzi Mafuruki kwa maneno na vitendo hasa kusikiliza maoni kutoka sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara hapa nchini,” amesema Kairuki.


Zinazohusiana:


Waziri huyo amesema Serikali inatambua mchango wake alioutoa katika kutengeneza ajira kwa Watanzania na kukuza uchumi kupitia miradi na makampuni aliyokuwa akimiliki. 

Mufuruki alikuwa anamiliki kampuni ya teknolojia ya Infotech Investment Group Limited na maduka ya Woolworth. Pia alikuwa muasisi wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Roundtable).

Mwenyekiti wa CEO Roundtable, Sanjay Roughani akithibitisha kifo cha mfanyabiashara huyo Desemba 8, 2019, alisema kuwa Mufuruki alianza kuugua akiwa Dar es Salaam na akapelekwa katika hospitali ya Agha Khan na kisha akapelekwa Afrika Kusini. 

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa na miaka 60 aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania na Wananchi Group Holdings.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW