Serikali kuzindua mradi wa Sh 99.8 bilioni kudhibiti magonjwa, dharura za afya
- Fedha za utekelezaji wa mradi huo zimetokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wadau wengine wa maendeleo.
Arusha. Serikali ya Tanzania inatarajia kuzindua mradi wa kitaifa wa kuimarisha uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kugundua, kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya mlipuko na dharura nyingine za afya Oktoba 15 mwaka huu.
Mradi huo unaojulikana kama “Pandemic Fund Project” unatarajia kutumia Sh99.8 bilioni na utazinduliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko, Jijini Mwanza.
Taarifa ya Dk Grace Magembe iliyotolewa leo Oktoba 13,2025 inabainisha kuwa fedha za utekelezaji wa mradi huo zimetokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wadau wengine wa maendeleo.
“Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 25 ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 61.2 za kitanzania…
…Aidha Kama ilivyo ainishwa mradi huu unatekelezwa kwa mashirikiano na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau wa maendeleo ambapo nyongeza ya kiasi cha fedha za kitanzania bilioni 38.7 kutoka Serikalini na wadau wa maendeleo kitatumika pia kufanikisha malengo ya mradi huu,” imesema taarifa Dk Magembe.
Wadau hao wa maendeleo watakaoshirikana na Tanzania katika utekelezaji wa maendeleo ni pamoja Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao).

Marburg ni miongoni mwa magonjwa ya mlipuko yaliyoikumba Tanzania mwaka 2025 yaliyohitaji dharura ya kiafya. Picha/CDC AFRICA.
Kupitia utekelezaji wa mradi huo, Serikali itaimairisha na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na utambuzi wa mapema na kuimarisha maabara za uchunguzi wa vimelea vya magonjwa.
Sambamba na hayo mradi huo utajenga uwezo wa wataalam na timu za dharura za afya, kuboresha uratibu wa dharura katika ngazi zote na kuimarisha mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii.
“Utekelezaji wa mradi huu utaimarisha ulinzi wa afya ya wananchi, kuongeza uthabiti wa jamii katika kukabiliana na dharura za afya na kuchangia moja kwa moja katika usalama wa afya wa kikanda na kimataifa,” imeongeza taarifa ya Dk Magembe.
Latest



