Serikali kuunganisha mwendokasi na uwanja wa ndege

January 16, 2026 4:02 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema hatua hiyo itarahisisha shughuli za usafiri na kukuza uchumi wa nchi.

Arusha. Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amesema mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi (BRT) Posta – Gongo la Mboto wenye killomita 23.6 utaunganishwa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ili kurahisisha huduma za usafiri.

Dk Nchimbi ameyasema hayo Leo Januari 16, 2026 wakati akifungua jengo maalum la viongozi mashuhuri katika uwanja huo jijini Dar es Salaam akisisitiza kuwa hatua hiyo itakuza uchumi wa nchi.

“Jitihada hizi kubwa zinalenga kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi kitaifa na kikanda, hii inatokana na fursa na faida za jiografia ya nchi yetu ambayo ni lango kuu la biashara kwa nchi zaidi ya nane,” amesema Dk Nchimbi.

Mbali na usafiri wa barabara, Nchimbi amesema Serikali itaunganisha njia nyingine za usafiri ikiwemo reli na viwanja mbalimbali vya ndege nchini ikiwemo Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Julius Nyerere, Msalato na kilimanjaro hatua itakayorahishsa zaidi usafiri na usafirishaji wa mizigo na bidhaa.

La kwanza Afrika Mashariki

Kwa mujibu wa Abdul Mombokaleo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), jengo hilo la viongozi limejengwa kwa miezi mitatu kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2025 chini ya mkandarasi CRJE East Africa Limited na timu ya wataalamu wa ndani likiwa na uwezo wa kubeba viongozi watano kwa wakati mmoja.

“Jengo hila la kisasa lenye ghorofa moja lina kumbi tano, mbili za marais, mbili za mikutano na moja ya kusubiria yaani waiting room…Hii inalifanya kuwa jengo la kwanza na la kipekee Afrika Mashariki,” amesema Mombokaleo.

Ujenzi wa jengo hilo ulitoa fursa za ajira kwa Watanzania 1,100 huku wengine wakinufaika na fursa za uuzaji wa kokoto, mchanga pamoja na nyenzo nyingine za ujenzi.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Makame Mbalawa, ujenzi wa jengo hilo utachochea kuimarika kwa huduma za viongozi na wakuu wa nchi watakaotembelea Tanzania, akiahidi kushirikiana na viongozi wengine kulitunza.

“Ninaomba nikuhakikishie jengo hili zuri na la kisasa tutalitunza ili liweze kuishi muda mrefu kama lilivyosanifiwa awali,” ameongeza Mbalawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks