Serikali kupunguza gharama ya kuchuja damu (dialysis)

August 15, 2025 8:52 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yawekeza Sh7.7 bilioni kufikia Agosti 2025
  • Yasema gharama ya kuchuja damu itashka hadi kufikia Sh100,000 au zaidi.

Arusha. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kufanya uwekezaji katika sekta ya afya kwa kuongeza madawa na vifaa tiba hatua inayotajwa kupunguza gharama za huduma za kuchuja damu (dialysis).

Gerson Msigwa, Msemaji Kuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Agosti 15, 2025  amesema Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ina lengo kupunguza gharama za kuchuja damu hadi Sh100,000.

“Mikakati tuliyonayo Serikali kupitia MSD ni kuendelea kushusha hizi gharama mpaka zifike S100,000 au chini ya hapo na inawezekana…

…Huko tunapokwenda tutafikia hatua ambayo mtu kuhitaji uchujaji wa damu itakuwa ni mahitaji ambayo wengi wanaweza kumudu,”amesema Msigwa.

Huduma ya uchujaji damu ni mchakato wa kimatibabu unaosaidia kusafisha damu kwa kuondoa sumu na maji ya ziada mwilini pale figo zinaposhindwa kufanya kazi yake ipasavyo. 

Wagonjwa wa figo huhitaji huduma hii mara moja mpaka mara tatu kwa wiki kutegemea na kiasi cha madhara kilichopo katika kiungo hicho muhimu mwilini jambo linalotajwa kuhitaji gharama kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa Msigwa gharama ya kuchuja damu kwa mara moja kwa sasa ni Sh200,000 iliyopungua kutoka Sh230,000 hadi Sh300,000 kwa miaka iliyopita.

Sambamba na kupunguza bei ya upatikanaji wa huduma hiyo Msigwa amebainisha kuwa Serikali iwekeza.Sh7.7 bilioni katika ununuzi wa.mashine za kuchuja damu na kuziongeza kutoka 60 zilizokuwepo hadi mashine 127 zilizonunuliwa kufikia Agosti mwaka huu.

Uwekezaji huo umesaidia kuongeza  idadi ya hospitali zilizopokea mashine kutoka MSD kwa ajili ya kuchuja damu kutoka sita zilizokiwepo awali hadi 15 mwaka 2025.

Miongoni mwa hospital zilizofikiwa na uwekezaji huo  wa mashine ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Morogoro na Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi.

Hospitali nyingine za rufaa zilizofikiwa na uwekezaji huo ni pamoja na Tumbi mkoani Pwani, Chato na Sekou Toure jijini Mwanza na Hospital ya Chuo Kikuu cha Dodoma huku nyingine nne zikiwa katika matengenezo.

“Hospitali nne zipo katika hatua ya matengenezo malengo yetu ni kwamba tuendee kupunguza gharama ya huduma hizi,”ameongeza Msigwa.

Aidha, Msigwa amewataka.Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji unaofaa ili kujilinda na ugonjwa wa figo ambao unazidi kishika kasi nchini. 

“Nawaomba Watanzania wazingatie elimu ya afya kwa sababu  ni sehemu kubwa ya maradhi haya tunayapata kwa kutozingatia kanuni za afya profesa Janabi akisema watu wengi wanambeza lakini anayoyasema ni muhimu kuliko ukisubiri uumwe ili ianze kutibiwa,”amesema Msigwa.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks