Jela miaka 100 kwa kukutwa na meno ya tembo, Mwanza

January 5, 2024 8:26 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni hukumu ya makosa matano tofauti ambapo kila kosa ni miaka 20 jela.
  • Miongoni ni kukutwa na nyara za Serikali pamoja na silaha kinyume cha sheria.

Mwanza. Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imewahukumu kifungo cha miaka 100 jela, watu watano kwa makosa matano tofauti likiwemo la kukutwa na meno saba ya Tembo.

Hukumu ya kesi hiyo ya kiuchumi namba 5 ya mwaka 2022, imetolewa jana Januari 4,2023 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Tumsifu Barnabas ambapo kila kosa kwa watuhumiwa likiwa na adhabu ya kifungo cha miaka 20.

Hakimu Barnabas amewataja waliohukumiwa kuwa ni a, Samson Emmanuel (48) Mkazi wa Ushirombo mkoani Geita, Mkazi wa Itigi mkoani Singida, Shalali Jisandu (40), Hamis Ngurumo (52), Mohammed Nasibu (32) na mkazi wa Doroto, Mathayo Robert (48).


Soma zaidi : Waziri Kairuki azindua kamati ya kitaifa ya kuongoa shoroba


Kwa mujibu wa Hakimu Barnabas, washitakiwa walifanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 86(1) na (2)(c)(iii) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori namba 283 ya mwaka 2002 ikisomwa pamoja na aya ya 14 na Kifungu namba 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi namba 200 ya mwaka 2022.

Washtakiwa hao walikutwa na hatia ya kukutwa na meno saba ya tembo pamoja na silaha ya bunduki aina ya G3.

“Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri katika shauri hili imejiridhisha pasi na shaka kwamba washtakiwa wana hatia na inawahukumu kwenda jela miaka 100 kila mmoja,” amesema Hakimu Barnabas.


Soma zaidi : Tanzania yachaguliwa makamu wa rais mkutano wa 25 wa UNWTO


Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi, Nyamhanga Mayagi, akisoma makosa yao, amesema kwa maeneo tofauti Julai 16,2022, walikutwa na meno saba ya tembo mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye thamani ya Sh138.9 milioni (USD 60,000).

Aidha,  walikutwa na silaha ya bunduki aina ya G3 ikiwa na risasi 3 kinyume cha kifungu namba 20(1)(a)(b) na 2 cha sheria ya Udhibiti wa Silaha na Vilipuzi namba 2 ya mwaka 2015, aya ya 31 na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi namba 200 ya mwaka 2022.

Enable Notifications OK No thanks