Serikali kudhibiti mifuko ya plastiki kwa wageni wanaoingia Tanzania

May 16, 2019 7:30 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Uamuzi wa kupiga marufuku mifuko ya plastiki ulitangazwa bungeni  Aprili 9, 2019 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwa ni hatua ya kulinda mazingira na kuchagiza matumizi ya mifuko mbadala inayotengenezwa kwa teknolojia rahisi. Picha|Mtandao.


  • Hawataruhusiwa kuingia na mifuko ya plastiki ya aina yoyote ifikapo June 1 mwaka huu.
  • Serikali kuanzisha vituo maalum vya ukaguzi mipakani na kwenye viwanja vya ndege. 

Dar es Salaam. Serikali imewataka wageni wote wanaokusudia kuingia nchini kuanzia Juni 1 mwaka huu kuzingatia marufuku ya kutokubeba na kutumia mifuko ya plastiki ikiwa ni hatua ya kutunza mazingira na kuhakikisha nchi inakuwa safi wakati wote. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Mei 16, 2019) na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, inaeleza kuwa aina zote za mifuko ya plastiki ya kubebea vitu bila kujali upana wake haitaruhusiwa kuingia, kusafirishwa, kutengenezwa, kuuzwa, kutunzwa, kusambazwa na kutumika Tanzania bara. 

Kutokana na marufuku hiyo, wageni wanaoingia nchini wanashauriwa kutokubeba mifuko ya plastiki katika mizigo yao ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa ukaguzi. 

“Wageni wanaoingia Tanzania wanashauriwa kuepuka kubeba mifuko ya plastiki au vifungashio vya plastiki katika mabegi au mizigo ya mkononi kabla ya kutembelea Tanzania,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Ili kuhakikisha zoezi hilo linapata mafanikio, Serikali inakusudia kuanzisha dawati maalum katika vituo vya kuingilia wageni ikiwemo mipakani na viwanja vya ndege vitakavyotumika kukagua wageni wanaoingia na mifuko ya plastiki. 


Soma zaidi: 


Hata hivyo, taarifa hiyo imeweka wazi kuwa marufuku hiyo haitahusu mifuko au vifungashio vya plastiki vinavyotumika katika huduma za afya, bidhaa za viwandani, sekta ya ujenzi na kilimo. Pia, mifuko inayotumika kuhifadhia chakula, usafi na takataka haitahusika. 

Pia mifuko inayofungwa kwa zipu (ziploc bags) ambayo ni maalum kwa kubeba vipodozi itaruhusiwa kwa sababu inabaki katika umiliki wa wageni kwa sababu haitarajiwi kutupwa nchini. 

Serikali imesema haikusudii kuona marufuku hiyo inawaletea tabu wageni wanaoingia nchini bali ni hatua muhimu inazochukua kulinda mazingira na kuweka nchi katika hali ya usafi na kupendeza. 

“Serikali inatarajia kuwa, wageni watakubaliana na usumbufu mdogo unaoweza kujitokeza wakati utekelezaji wa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki,” inaeleza taarifa hiyo. 

Uamuzi wa kupiga marufuku mifuko ya plastiki ulitangazwa bungeni  Aprili 9, 2019 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikiwa ni hatua ya kulinda mazingira na kuchagiza matumizi ya mifuko mbadala inayotengenezwa kwa teknolojia rahisi. 

Ikiwa marufuku hiyo itaanza kutumika kama ilivyopangwa, Tanzania itaungana na nchi za Rwanda, Kenya pamoja na Zanzibar ambazo tayari zimezuia mifuko ya plastiki katika nchi zao. 

Enable Notifications OK No thanks