Makamba awatahadharisha wafanyabiashara wanaendelea kununua mifuko ya plastiki

April 30, 2019 10:39 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema wakiendelea kununua kwa ajili ya kuiuza kabla ya Juni 1 itawadodea.
  • Marufuku hiyo haitahusisha mifuko ya plastiki ya kukusanyia taka (trash bags).

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba amewaonya wafanyabiashara wa mifuko ya plastiki kutoendelea kununua bidhaa hizo ili zisiwadodee ikiwa umesalia mwezi mmoja kuanza kwa marufuku ya matumizi ya mifuko hiyo hatari kwa mazingira.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter, Makamba ameeleza kuwa tarehe ya mwisho ya matumizi ya mifuko hiyo ya plastiki itakuwa Juni Mosi na wala siyo Mei Mosi kama ambavyo habari hiyo inavyosambazwa mtandaoni.

“Siku ya mwisho ni tarehe 1 Juni 2019 ambapo adhabu kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji zitaanza kutumika. Kama una duka/genge usiendelee kununua mifuko. Itakudodea,” ameeleza Makamba.

Hata hivyo, katika kujibu baadhi ya maswali ya watumiaji mifuko hiyo nchini mtandaoni, Makamba amesema zuio hilo la matumizi ya mifuko ya plastiki halitahusisha mifuko ile inayotumika kukusanyia taka katika ndoo za takataka maarufu kwa Kiingereza (trash bags).

Amesema mifuko ni minene kidogo jambo linalofanya iwe rahisi kurejereshwa kiwandani kama ilivyo mifuko ile inayotumika katika shughuli za ujenzi. 


Zinazohusiana:


Kupigwa marufuku kwa mifuko hiyo laini ya plastiki nchini kunafungua fursa adhimu kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaozalisha mifuko mbadala kama ile ya karatasi, nguo na malighafi nyinginezo ambazo ni rahisi kuoza au kurejelezwa (Recycled). 

Tanzania inaungana na mataifa mengine ulimwenguni zaidi ya 60 ambayo yamepiga marufuku kabisa au sehemu ya mifuko hiyo kama Kenya, China, na Ufaransa. 

Visiwani Zanzibar pia hakuna matumizi ya mifuko hiyo ya plastiki ambayo imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa uchafu mitaani na baharini nchini. 

Enable Notifications OK No thanks