Serikali kuanzisha mamlaka mpya ya Tiseza kuchochea uwekezaji
- Itachukua nafasi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji Tanzania
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inakusudia kuanzisha Mamlaka mpya ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) ili kuchochea kasi ya uwekezaji mpya, kuuendeleza na kuusimamia vyema.
Mamlaka hiyo itaundwa kwa kuunganisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji Tanzania (EPZA), jambo linalotarajiwa kuongeza kasi ya uwekezaji kwa kupunguza urasimu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo aliyekuwa akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi wa 2024 bungeni jijini Dodoma amewaambia wabunge kuwa chimbuko la muswada huo ni kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuziunganisha taasisi hizo mbili.
Kitila amesema kuwa kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mpya kutaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani, ilidhamiria kukuza uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara kama sehemu muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi nchini,” amesema Prof Mkumbo.
Aidha, Prof Mkumbo alibainisha kuwa, mswada huo una malengo ya kuweka masharti ya uendelezaji wa uwekezaji Tanzania, kuweka masharti ya mazingira bora kwa wawekezaji, na kuweka mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu, ulinzi na uvutiaji uwekezaji.
Kwa mujibu wa Kitila muswada huo unapendekeza maboresho makubwa katika sekta ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na fursa na vivutio kwa wawekezaji wa ndani kwa kuweka vivutio mahsusi kwa wawekezaji wa ndani pekee.
Pia muswada huo ambao umeshapitishwa na Bunge unapendekeza kuanzishwa kwa benki ya ardhi ambayo itahusika na kutenga maeneo ya uwekezaji, huku watu binafsi na makampuni wakiruhusiwa kusajili ardhi zao kwa ajili ya uwekezaji.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walichangia juu ya mswada huo akiwemo Haji Omary amebainisha kuwa njia zilizotumika kupendekeza mswada huo ni njia bora za ushirikishaji kwa kuangalia maeneo mazuri.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Mwibara Charles Kajege ameshauri watumishi watakao kuwa kwenye mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa wanakuwa mbele ya wakati ili kutambua vivutio na kujua namna ambavyo watapata wawekezaji.

“Inabidi watumishi wa mamlaka hii wapate nafasi za kwenda kujifunza katika mamlaka ya nchi nyingine…hii itasaidia watumishi wetu kuwa mbele ya wakati. Mimi nashauri Serikali pamoja na mambo mengine ihakikishe kwamba watumishi wa mamlaka yetu hii wawe na uwezo wa kuongea lugha nyingi za kigeni,” ameeleza Kajege.
Licha ya kuunga mkono mswada huo Mbunge wa viti maalum kutoka mkoa wa Mwanza Mary Masanja amesisitiza kuwa suala la utoaji wa ardhi liwe na mchakato ya kuwafanya wazawa kulipwa fidia kwa wakati na kuwepo kwa mfumo mzuri kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje.
Latest



