Bunge lashauri kuimarishwa idara ya kushughulikia wakimbizi Tanzania

February 6, 2025 4:33 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Lasema itasaidia  kuepusha nchi na  athari hasi za kiuchumi, kijamii na kiusalama.

Dar es salaam. Bunge la Tanzania limeishauri Serikali kuboresha idara ya kusimamia wakimbizi kwa kuifanya kuwa mamlaka inayojitegemea ili isimamie kwa ufanisi changamoto zinazohusiana na wakimbizi ikiwemo kudhibiti wakimbizi kutoroka na kuishi nje ya kambi kinyume na sheria.

Pendekezo hilo limetolewa bungeni jijini Dodoma leo Februali 6, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa ambaye amesema idara hiyo ipewe uwezo wa kusimamia rasilimali zake na kujitegemea badala ya kutegemea fungu la bajeti la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kawawa ameongeza kuwa kutegemea bajeti kutoka wizarani kunasababisha idara hiyo kuwa na mapungufu ya kifedha na jambo linalozuia utekelezaji kamili wa majukumu ya idara hiyo. 

“Iwe idara inayojitegemea na kujiendesha kwa namna inayowezesha kusimamia masuala ya wakimbizi, iwezeshewe upatikanaji wa fungu la kibajeti kwa idara ya wakimbizi tofauti na sasa ambapo idara hiyo inapata fedha zake kupitia fungu 51 la wizara, na Serikali itenge fungu la kutosha kwa idara ya wakimbizi ili iweze kutekeleza majukumu yake kama ilivyokusudiwa,” amesema Kawawa.

Kwa mujibu wa  ufuatiliaji na uchambuzi wa kamati hiyo kuna idadi kubwa ya wakimbizi wanaoishi nje ya kambi rasmi kinyume na sheria na taratibu za kimataifa. 

Wakimbizi hao wamejipenyeza kwenye jamii na kuendesha shughuli za kiuchumi kama wananchi wa kawaida katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na Tabora, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tanga, Geita, na Kagera.

Itakumbukwa Januari 22, 2024 Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) wa Tanzania, Jenerali Jacob Nkunda, alisema kuwa wapo watu waliokuja kama waomba hifadhi au wakimbizi na sasa wameteuliwa katika nafasi za kufanya maamuzi baada ya kukaa nchini kwa muda, hali ambayo ameieleza kuwa hatari inayoweza kuathiri usalama. 

Nkunda alieleza kuwa kati ya Januari 1 na Disemba 31, 2023, wakimbizi 138,149 waliingia nchiniw engi wao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC Congo) na Burundi, wakitafuta fursa bora za kiuchumi kama malisho ya mifugo sababu ambazo hazikubaliki kama sababu ya kuomba hifadhi.

Rais Samia alijibu kuhusu hali hiyo kwa kusema kwamba Serikali imepokea onyo kuhusu kuwahudumia wakimbizi nchini na wanatafuta njia za kuwarudisha katika nchi zao pamoja na kubainisha kuwa hivi karibuni uwezo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) umepungua na kwamba nchi itatafuta njia za kushirikiana na nchi jirani kuhusu suala hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa akisoma taarifa ya kamati bungeni. Picha |Bunge la Tanzania

Kwa mujibu wa takwimu za UNHCR, hadi kufikia Desemba 31, 2024, Tanzania inahifadhi wakimbizi na waomba hifadhi 230,689, hasa kutoka nchi majirani zinazokabiliwa na mapigano za Burundi na DR Congo. 

Takriban asilimia 83 yaani wakimbizi 189,696 wanaishi katika kambi mbili za Nduta na Nyarugusu zilizoko Kigoma huku wengine 40,993 wakiwa kwenye kambi za Katumba, Ulyankulu, Mishamo, Dar es salaam na Chogo.

Tofauti na wakimbizi hawa walioko kwenye kambi kihalali, uwepo wa wengine nje ya kambi hizo maalumu ni hali iliyo kinyume na sheria za ndani na kimataifa zinazosimamia masuala ya wakimbizi. 

Hata hivyo, changamoto kuu zinazokabili Serikali kwa mujibu wa Kawawa ni upungufu wa rasilimali watu na fedha kwa idara ya huduma za wakimbizi, pamoja na ukosefu wa mfumo maalum wa kufuatilia wakimbizi walio nje ya makambi. 

Aidha, Kawawa ameongeza kuwa wananchi hawana mwamko wa kutoa taarifa kuhusu wakimbizi waliojipenyeza kwenye makazi yao ambao wameshakaa kwa muda mrefu na sasa wanaonekana kama watu wa jamii hiyo ambapo wanaendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi.

Miongoni mwa athari za wakimbizi kutokuishi ndani ya utaratibu uliopo kisheria ni baadhi yao husasan watoto kukosa haki za msingi kama elimu kwa sababu ya wazazi wao kuhofia kuwaandikisha ili kutotambulika na mamlaka za Serikali.

Endapo pendekezo hilo la Bunge litafanyiwa kazi na ukafanyika uchunguzi wa kina kubaini wakimbizi waliopo nchini kinyemela huenda Tanzania ikafanikiwa kukabiliana na changamoto za wakimbizi waishio nchini kinyume na sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks