Safari ya Ufaransa iliyoniachia funzo kubwa kuhusu kumbukumbu

August 5, 2022 1:58 pm · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Wananchi wa nchi hiyo wamejijengea mazoea ya kutunza vitu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
  • Zinawasaidia kujua walikotoka, walipo na wanakokwenda.

Dar es Salaam. Mapema mwezi wa Julai 2022 nilibahatika kuiwakilisha Tanzania nchini Ufaransa katika programu ya vijana wanaozungumza lugha ya Kifaransa iliyoandaliwa Lions Club France.

Kwa takribani mwezi mmoja nilikuwa Ufaransa katika Ukanda wa Bourgogne-Franche-Comté nikiendelea na shughuli zilizonipeleka.

Programu hii ya mafunzo huwakutanisha vijana ambao wanazungumza Kifaransa na kujadili masuala mbalimbali kama urithi, tamaduni, sanaa, asili na mazingira.

Safari yangu nchini Ufaransa nimeweza kujifunza mambo mbalimbali lakini jambo kubwa ambalo limenivutia ni namna wa watu wa Taifa hilo la Ulaya lilivyofanikiwa kujenga utamaduni wa kuhifadhi na kutunza kumbukumbu ya vitu mbalimbali vikiwemo vya kihistoria.

Katika matembezi yangu ambayo ninaweza kuyaita ya kitalii nilishuhudia vitu magari ya zamani, vitabu, nyumba za kale na mashine zilizotumika enzi za mapinduzi ya viwanda barani Ulaya hasa nchini Ufaransa vimetunzwa hadi leo ili watu waweze kujifunza na kujua historia.

Uhifadhi na utunzaji wa kumbukumbu wa vitu mbalimbali ni tabia ambayo ipo miongoni mwa wananchi wa Ufaransa, jambo ambalo linasaidia historia ya Taifa kurithishwa vizazi hadi vizazi.

Kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, familia hadi kitaifa,  utagundua kuwa uhifadhi na utunzaji wa kumbukumbu ni jambo ambalo limeshamiri kwani hutumika kama rejea katika historia.

Kumbukumbuku hizo utazikuta katika maandishi na majengo na vitu vinavyodhaniwa vina umuhimu huifadhiwa sehemu salama. 

Nilibahatika kutembelea makumbusho ya Châtillon inayopatikana mji wa Châtillon-sur-Seine katika Ukanda wa Bourgogne-Franche-Comté hapa nilikuta nyaraka mbalimbali zilizotunzwa na kuhifadhiwa likiwemo birika kubwa lililotumiwa na watawala wa Kigiriki. 

Birika hilo linakadiriwa kuwa na miaka 2500 ambalo lilikuwa likitumika kuwekea maji na wakati mwingine mvinyo.

Kitabu chenye maandishi yaliyoandikwa kwa lugha ya Kilatini  kikiwa kimehifadhi kwenye maktaba ya Gray katika mji wa Châtillon-sur-Seine nchini Ufaransa. Picha| David Mselewa.

Moja ya sehemu ambayo pia nilibahatika pia kutembelea ni katika maktaba ya Gray inayopatikana katika mji wa Gray en Haute-Saône ambayo ilianzishwa mwaka 1859. 

Maktaba hii imetunza nyaraka mbalimbali vikiwemo vitabu ambavyo vimeandikwa kwa miaka mingi huku moja ya nyaraka maarufu katika maktaba hiyo ni kitabu chenye maandishi ya lugha ya Kilatini ambacho kiliandikwa katika karne ya 13.

Hayo na mengine utayakuta katia kila kona ya Taifa hilo ambalo pia watu wake wanapenda kusoma na kujifunza mambo mbalimbali na historia ya walikotoka ili kujenga maisha bora ya wanakokwenda. 

Kila mtu ni balozi wa kutunza kumbukumbu

Ikiwa familia ndiyo msingi wa jamii na jamii ndiyo hujenga taifa, basi si ajabu kuona tabia ya uhifadhi na utunzaji wa kumbukumbu miongoni mwa familia nchini Ufaransa.

Katika safari hii nilibahatika kuishi na familia ya Wafaransa kwa wiki moja katika kijiji kinachoitwa Monberthault, hapa napo nilishuhudia namna uhifadhi na utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali ikiwemo vifaa na nyaraka zilivyotunzwa na familia hiyo.

Siku moja katika mlo wa jioni na wenyeji wangu pamoja na marafiki wengine, baba mwenye nyumba alitoa ala ya muziki iitwayo Accordion kwa lugha ya Kingereza na alipiga ala hiyo.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 73 alisema kuwa kifaa hicho alikuwa anakitumia ujanani na wakati mwingine kwa umma na hivyo kujipatia pesa ambayo ilimsaidia katika masomo yake akiwa shuleni.

Hili ni jambo zuri kuona kifaa hicho kimekaa kwa miaka yote tangu ujana mpaka uzeeni.

Hawa watu hawatupi nyaraka kwa sababu kwao ni mali. Risiti za manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali huifadhiwa sehemu nzuri kwa sababu huzisaidia familia zao kufanya rejea pale itakapobidi.

Nimehitimisha safari hii huku nami nikiwa na shauku ya kutaka kuhifadhi na kutunza kumbukumbu za vitu vyangu ili vizazi vyangu baadaye nao waweze kujifunza.

Kasri ya Bussy-rabutin inayopatikana katika mji wa Bussy- le grand nchini Ufaransa ambalo kwa sasa linatumika kama makumbusho. Picha| David Mselewa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW