Sababu Tanzania kuadhimisha Siku ya Mashujaa Julai 25
- Ni baada ya kurejea kwa askari waliokuwa vitani nchini Uganda
- Awali ilikuwa ikiadhimishwa Septemba mosi kila mwaka
Dar es Salaam. Kila ifikapo Julai 25 nchi ya Tanzania huadhimisha Siku ya Mashujaa ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda uhuru wa Tanzania.
Kikawaida siku hii huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalum ya kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha na kuiombea amani nchi kutoka kwa viongozi wa dini pamoja na hayo hufanyika gwaride maalum kwa ajili ya mashujaa waliopoteza maisha.
Hata hivyo kabla ya mwaka 1979 siku hii haikuwa ikiadhimishwa Julai 25, kila mwaka badala yake yalikuwa yakifanyika kila ifikapo Septemba Mosi, siku ambayo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianzishwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) siku hiyo ilibadilishwa ikiwa ni kuwaenzi askari waliorejea Julai 25, 1979 baada ya mashujaa waliokwenda kushiriki vita nchini Uganda kurejea na kupokelewa eneo la Bunazi mkoani Kagera na muasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwenye kumbukumbu ya siku ya mashujaa kitaifa pichaI Ikulu
Leo Julai 25, 2024 maadhimisho ya siku hii yamefanyika katika uwanja wa mashujaa, Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.
Hii ni kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo kufanyika katika uwanja wa mashujaa tangu Rais Samia alipoamugiza Waziri Mkuu mwaka 2022 kutafuta eneo la kujenga mnara wenye hadhi ya makao makuu ya nchi ambapo leo aliweka ngao na mkuki katika mnara huo.
Soma zaidi: Rais Samia arejesha tena sherehe za mashujaa, akiagiza wajengewe mnara Dodoma
Mnara huo unaoendelea kujengwa unatarajiwa kuwa wa kwanza kwa urefu nchini Tanzania ikiwa ni nembo ya kuendelea kuwaenzi mashujaa waliopoteza maisha wakati wanatetea na kupigania uhuru wa Tanzania.
Latest
