Rais Samia arejesha tena sherehe za mashujaa, akiagiza wajengewe mnara Dodoma
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kwenye Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma Julai 25, 2022. Picha| Ikulu.
- Sherehe hizo zilisimama tangu mwaka 2016 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Uviko-19.
- Aagiza mashujaa hao wajengewe mnara mkubwa Dodoma.
Dar es Salaam. Baada ya kutofanyika kwa miaka mitano kwa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Uviko-19, Rais Samia Suluhu Hassan amesema sherehe hizo zitaendelea kuadhimishwa kama kawaida huku akiagiza kujengwa kwa mnara mkubwa wa mashujaa mkoani Dodoma.
Mara ya mwisho sherehe za maadhimisho ya siku ya mashujaa zilifanyika Julai 25 mwaka 2016 Mkoani Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli.
Katika kipindi hicho, sherehe hizo zilikuwa zinaadhimishwa kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya usafi, kutoa huduma za tiba bure katika vituo vya afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Tanzania.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya siku ya Mashujaa kitaifa yaliyofanyika leo Julai 25 2022 jijini Dodoma katika viwanja vya Mashujaa amesema nchi itaendelea kuadhimisha siku hiyo ili kuthamini ma kuenzi mchango wa wapigania uhuru wa Tanzania.
“Kwa miaka ya hivi karibuni hatukuweza kukutana kwanza kwa lile janga lilioikumba dunia la Uviko-19,lakini, leo Mungu ametujalia tumeweza kukutana na tutaendelea kukutana siku zijazo,” amesema Rais Samia.
Amesema mchango wao mkubwa ndiyo unaoifanya Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani na inayofuata misingi ya utawala bora.
Soma zaidi:
-
Wiki ya Maji: Wadau wanavyookoa mazingira ya Ziwa Victoria
-
Mwanza ilivyojipanga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama
Kutokana na sherehe hizo kuadhimishwa katika jiji la Dodoma ambako ndiko makao makuu ya nchi Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka kutafuta eneo kubwa na bora zaidi litakalojengwa mnara wa mashujaa wenye hadhi ya makao makuu ya nchi kwa gharama nafuu.
“Nipendekeze kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yako pamoja na mkuu wa mkoa wa Dodoma kutafuta eneo kubwa na bora zaidi kujenga mnara wewnye hadhi ya makao makuu ya nchi kwa gharama zitakazostahimilika,” amesema Rais.
Muda mfupi baada ya Rais kutoa agizo, Majaliwa amekutana na watendaji wake kujadili mchakato wa kuanza kujenga sanamu hiyo.
Waziri Mkuu @KassimMajaliwa_ leo Julai 25, 2022 ameitisha kikao cha kujadili utelekezaji wa agizo la Rais @SuluhuSamia alilolitoa katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu itafute eneo utakapojengwa mnara mpya wa mashujaa wenye hadhi ya Makao Makuu. pic.twitter.com/nOU3mwbLON
— Ofisi ya Waziri Mkuu (@TZWaziriMkuu) July 25, 2022
Siku ya mashujaa ni nini?
Kwa mujibu wa tovuti ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Siku ya Mashujaa ni siku ya kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda uhuru wa Tanzania kila ifikapo Julai 25 ya kila mwaka.
“Siku hii ya kuwakumbuka mashujaa huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalum ya kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha na kuiombea amani nchi kutoka kwa viongozi wa dini. Pamoja na hayo hufanyika gwaride maalum kwa ajili ya mashujaa wetu” inasomeka sehemu ya andiko hilo,” imeeleza sehemu ya tovuti ya JWTZ.
Aidha, Rais ametumia pia fursa ya maadhimisho hayo kuwakumbusha Watanzania kuendelea kupata chanjo ya Uviko-19 ili kujilinda na ugonjwa huo ambao bado haujaisha pamoja na kujitokeza katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu.
Latest
