Mfahamu Brigedia Mndolwa shujaa aliyepigana vita vya Kagera

July 25, 2025 5:57 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Alihudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Burundi jijini Bujumbura mwaka 2003 hadi 2010.
  • Brigedia Jenerali Mndolwa alistaafu rasmi jeshini kwa heshima Februari16, 2014.

Dar es Salaam. Katika historia ya Tanzania yapo majina machache yanayobeba alama ya uzalendo wa kweli na moyo wa kujitoa kwa ajili ya Taifa.

Miongoni mwao ni Balozi Brigedia Jenerali mstaafu Francis Benald Mndolwa, shujaa aliyeweka maisha yake rehani kulinda mipaka ya nchi dhidi ya majeshi ya uvamizi ya Idi Amin wa Uganda katika vita vya Kagera mwaka 1978.

Kwa kutambua mchango wake katika kulinda na kutetea maslahi ya Taifa Brigedia Mndolwa aliweka mfano wa shoka kwenye mnara wa Mashujaa katika mji wa Serikali Mtumba, Dodoma akiwakilisha mashujaa wa Vita vya Kagera katika maadhimisho ya siku hiyo leo Julai 25, 2025.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa Mtumba Jijini Dodoma akiwemo Brigedia Mndolwa. Picha/ Ikulu Mawasiliano.

Brigedia Mndolwa  alitekeleza jukumu hilo mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo, akifuatana na viongozi wengine wa kitaifa akiwemo Makamu wa Rais, Philip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Ali Mwinyi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko. 

Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika picha. Picha/ Ikulu mawasiliano.

Kila ifikapo Julai 25 nchi ya Tanzania huadhimisha Siku ya Mashujaa ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kuulinda uhuru wa Tanzania.

Kikawaida siku hii huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalum ya kuwaombea mashujaa waliopoteza maisha na kuiombea amani nchi kutoka kwa viongozi wa dini pamoja na hayo hufanyika gwaride maalum kama heshima Kwa  mashujaa waliopoteza maisha.

Mfahamu Brigedia Mndolwa

Balozi Brigedia Mndolwa alizaliwa Februari 17, 1946 katika Kijiji cha Ubiri Lushoto, mkoani Tanga, na alianza elimu yake ya msingi mwaka 1955 hadi 1962, kisha kujiunga na shule ya sekondari ya Mtakatifu Francisco, Pugu kuanzia kidato cha kwanza mwaka 1963 hadi kidato cha sita mwaka 1968.

Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  Juni 10, 1969, akianzia mafunzo ya msingi ya kijeshi na baadaye kupanda ngazi kwa bidii na weledi.

Brigedia Mndolwa, alihitimu kozi ya kamisheni mwaka Novemba 1970 na kuwa Kamanda wa Platuu mwaka 1973.

Mwaka 1974 Brigedia Mndolwa alikuwa Kamanda wa Kombania nchini Pakistani na baadae kamanda wa uratibu nchini Nigeria mwaka 1987.

Katika utumishi wake wa kijeshi, alishika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Kamanda wa Kikosi cha tano (5 Batuliani), Meja na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea.

Wakati wa Vita vya Kagera, Brigedia Mndolwa alirudishwa jeshini kuongoza kikosi chake katika medani ya ‘Seattle Front’. 

Akiwa katika vita hivyo mwaka 1978 hadi 1979, Brigedia Mndolwa aliongoza operesheni maalum za kijeshi na kufanikisha kuondoa majeshi ya adui katika maeneo ya Butiama, Boko, Dongo na Kasongola maeneo ambayo yalikuwa chini ya mashambulizi makali ya anga kutoka kwa majeshi ya Idi Amin.

Baada ya vita, kufuatia agizo la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, la kuwarejesha wanajeshi katika nafasi zao za kiraia, Brigedia Mndolwa aliteuliwa tena kuwa Mkuu wa Mkoa wa Nachingwea na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa huo.

Kwa mchango wake mkubwa, alitunukiwa nishani kadhaa za heshima ikiwemo nishani ya vita ya Kagera, nishani ya miaka 20 ya JWTZ, na  nishani ya utumishi uliotukuka.

Balozi Jenerali Mstaafu Francis Bernard Mndolwa akielekea kuweka mfano wa shoka wakati akiwawakilisha Mashujaa wa Vita vya Kagera kwenye mnara wa Mashujaa katika mji wa serikali Dodoma. Picha /Ikulu Mawasiliano

Kuanzia mwaka 2003 hadi 2010, alihudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Burundi jijini Bujumbura.

Brigedia Jenerali Mndolwa alistaafu rasmi jeshini kwa heshima Februari 16, 2014, baada ya kulitumikia Taifa kwa moyo wa kujitolea na uadilifu kwa muda wa miezi 10 na siku 6 akiwa katika cheo chake cha mwisho.

Leo, katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa historia yake inabaki kuwa somo la uzalendo, ujasiri na kujitoa kwa dhati kwa ajili ya Taifa. 

Brigedia Mndolwa ni mfano wa kweli wa askari aliyepigana si kwa ajili ya umaarufu, bali kwa ajili ya amani ya Watanzania wote.

Rais wa Tanzania na Samia Suluhu Hassan akishiriki maadhimisho ya Siku ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma. Picha/ Ikulu Mawasiliano.

Habari hii imeandikwa na Fatuma Hussein, Sauda Ndaza na kuhaririwa na Lucy Samson.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV