Sababu balozi za nje kuchelewa kuhamia Dodoma
- Mpaka sasa ni balozi tatu ndiyo zimefungua ofisi Dodoma.
- Serikali yasema huenda mipango ya fedha ikawa sababu.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutenga maeneo katika jiji la Dodoma kwa ajili ya kujenga ofisi za balozi mbalimbali zinazowakilisha nchi zao Tanzania, ni balozi tatu tu zimefanikiwa kujenga ofisi zao katika jiji hilo ambalo ndiyo makao makuu ya nchi.
Serikali ya Tanzania ilihamishia shughuli zake za kiserikali rasmi Dodoma Julai 2016 na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Hayati John Magufuli ambapo iliagiza watumishi wa umma na taasisi za kimataifa kuhamia jijini humo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nchi zilizofanikiwa kufungua ofisi za balozi zao ni Uingereza, Ujerumani na China.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Godfrey Pinda akizungumza leo Mei 16, 2022 kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika amesema baadhi ya balozi kushindwa kuhamia kwenye mji mkuu huo kuwa ni kutokuwa na mipango ya kifedha kufanikisha suala hilo.
“Ni suala la kila nchi kujiwekea mpango wa uhamisho ambao unahitaji fedha, upo uwezekano mkubwa sana wa nchi nyingi kudelay (kuchelewa) kuhamia hapa Dodoma kwa sababu ni lazima ziingie kwenye mpango wa fedha na kuruhusu balozi zao zihamie dodoma,” amesema Pinda.
Pinda alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala aliyetaka kujua sababu za baadhi ya balozi kushindwa kuhamishia ofisi zao Dodoma.
Soma zaidi:
Katika mipango yake, Serikali imetenga eneo la heka tano kwenye jiji la Dodoma kwa kila balozi zenye uwakilishi nchini kujenga makazi ya ofisi zao.
Licha ya balozi hizo kusua sua kuhamia Dodoma, baadhi ya jumuiya za kimataifa zimefungua ofisi zao katika mkoa huo uliopo katikati mwa Tanzania likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN WOMEN).
Mashirika mengine ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (IOM), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada (UN AID).
Ikiwa taasisi za kimataifa zitaongeza kasi ya kuhamia Dodoma, itaisaidia kuendelea kuufungua Mkoa wa Dodoma kibiashara na kuwainua kiuchumi wananchi wa mkoa huo.
Pia itaweza kutekeleza kikamilifu ndoto ya muda mrefu ya baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kuhamishia shughuli za kiserikali Dodoma.
Latest
