Ruto ambwaga Odinga urais Kenya baada ya kupata asilimia 50.49 ya kura

August 16, 2022 5:12 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Aahidi kufanya kazi kwa kuzingatia demokrasia, uwazi na uadilifu
  • Wakenya waaswa kutunza amani yasijirudie ya 2007

Dar es Salaam. Baada ya mchuano mkali katika vituo vya kuhesabu kura hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Huru na Mipaka nchini Kenya (IEBC) Wafula Chebukat Kenya amemtangaza William Ruto kuwa mshindi wa kiti cha urais na kuwa Rais mteule wa awamu ya tano.

Matokeo ya uchaguzi huo wa aina yake yalikuwa yakisubiriwa kwa hamu na mamilioni ya watu ulimwenguni kote kutokana na ushindani mkali uliokuwepo kati ya wagombea wawili ambao ni Raila Odinga wa muungano wa Azimio na William Ruto aliyeibuka mshindi kutoka muungano wa Kenya Kwanza. 

Rais mteule wa Kenya, William Ruto alichuana vikali na mpinzani wake wa karibu Raila Odinga na kumwaga kwa ushindi mwembamba baada ya kuweka kibindoni asilimia 50.49 ya kura dhidi ya asilimia 48.5 za mpinzani wake. Picha|William Ruto/Twitter. 

William Ruto ameibuka na ushindi kwa kupata kura 7.176 milioni ( 7,176,141) ambazo ni sawa na asilimia  50.49 huku mshindani wake  wa karibu Raila Odinga akipata kura 6.942 milioni (6,942,930) ambayo ni sawa na asilimia  48.5 ya kura halali zilizopigwa. Matokeo hayo sasa yamemfanya Ruto kuwa rais mteule wa taifa hilo la Afrika Mashiriki.

“Kwa mujibu wa katiba na sheria mimi Wafula Chebukati mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Huru na Mipaka ninatamka kwamba Ruto William Samoei amechaguliwa kama Rais wa  Jamhuri ya Kenya kufuatia uchaguzi uliofanyika Agosti 9,” amesema Chebukati huku akisaini cheti cha matokeo ya urais.

Majaribio ya kudukua mifumo ya kuhesabu kura ni miongoni mwa mambo yaliyochelewesha kutangazwa kwa matokeo hayo yaliyotarajiwa kutolewa majira ya saa tisa alasiri, hata hivyo baada ya wadukuzi kudhibitiwa matokeo yalitangazwa majira ya saa 12:00 jioni.

Kabla ya kutangazwa matokeo hayo, zilitokea vurugu katika ukumbi ambapo baadhi ya watu waliokuwemo katika eneo hilo “kuzichapa kavukavu.” 

Katika salamu zake baada ya kutangazwa mshindi,  Ruto ambaye alikuwa makamu wa Rais wa awamu ya nne Uhuru Kenyatta, amesema atafanya kazi na wote waliochaguliwa huku akiahidi kuboresha demokrasia.

“Naahidi nitafanya kazi kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia demokrasia, nampongeza mpinzani wangu Odinga na tutafanya kazi kwa kushirikiana,” amesema Ruto.


Hata hivyo, Odinga hakuonekana katika ukumbi huo wa Bomas uliopo jijini Nairobi.  

Licha ya Ruto kutangazwa mshindi, matokeo ya uchaguzi huo yametangazwa kukiwa na mpasuko baina ya makamishna wa IEBC huku wengine wakisema hawakubaliani na matokeo hayo kutokana na dosari zilizojitokeza katika hatua ya matokeo. 

Wakenya wamesubiri matokeo hayo kwa siku saba baada ya kupiga kura Agosti 9 mwaka huu katika kampeni zilizovuta mamia ya watu nchini humo. 

Itakumbukwa kuwa historia ya kenya iliingia dosari mwaka 2007 mara baada ya kutokea machafuko yaliyosababisha zaidi ya watu 1,000 kuuwawa na wengine 300,000 kuachwa bila makazi kutokana na vurugu zilizozuka mara baada ya matokeo ya Urais kutangazwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW