Ripoti ya ajali ya ndege Precision Air yaeleza kuchelewa boti, aliyefungua mlango
- Yaeleza aliyehusika kufungua mlango ni mhudumu wa ndege kwa kushirikiana na abiria.
- Boti ya uokozi ilifika wakati zoezi la uokoaji limekamilika kwa kuwa ilikuwa kwenye doria.
Dar es Salaam. Serikali imekiri kuwa boti rasmi ya uokoaji ndani ya Ziwa Victoria ilichelewa kufika eneo la ajali ya ndege ya Precision Air iliyoua watu 19 mapema mwezi huu baada ya kuwepo mjadala mkubwa juu ya uwepo wa uzembe katika uokozi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa, aliyekuwa akisoma ripoti ya awali ya ajali ya ndege hiyo aina ya ATR 42-500, amewaambia wanahabari kuwa katika eneo hilo kuna boti ya uokozi moja ambayo wakati ajali inatokea ilikuwa mbali na uwanja wa ndege wa Bukoba ikifanya doria.
“Kwa kuwa ilikuwa mbali, ilipofika katika uwanja wa ndege shughuli za uokoaji zilikuwa zimekamilika,” amesema Prof Mbarawa.
Tangu ajali hiyo itokee Novemba 6 wadau wamekuwa wakiikosoa vikali Serikali namna ilivyoshughulikia uokozi katika ajali hiyo ambayo watu 24 walinusurika baada ya ndege kuanguka majini wakati ikitua katika uwanja wa Bukoba.
Wakati wa uokoaji baadhi ya waokoaji walikuwa wakiivuta ndege hiyo na kamba huku wavuvi wa eneo hilo wakifanya shughuli kubwa ya uokozi.
“Ajali hii haikutarajiwa, ajali ni ajali. Inapotokea ajali kila wadau mbalimbali hushiriki kukabiliana nayo. Serikali ilifanya kila linalowezekana katika kukabiliana na ajali hii,” amesema Prof Mbarawa.
Katika mkutano huo na wanahabari, waziri huyo amesema anatambua kuwa uwezo wa kukabiliana na ajali na majanga unatakiwa kuimarishwa zaidi.
“Ripoti hii ya awali tumeipokea na ripoti nyingine tutazipokea na kuzifanyia kazi,” amesema Prof Mbarawa leo Novemba 24, 2022.
Serikali yaikana ripoti iliyovuja
Usiku wa Jumanne ilisambaa mtandaoni ripoti inayodaiwa kuwa ni ripoti ya awali ya uchunguzi wa ndege hiyo ikieleza kuwa “iwapo hatua za haraka za uokozi zingefanywa huenda watu wengi wangeokolewa” jambo lililozua mjadala mkubwa mtandaoni na vyombo vya habari.
Serikali imeikana ripoti hiyo ikieleza kuwa si rasmi kwa kuwa haikutolewa na mamlaka husika na wala Prof Mbarawa mwenyewe haikusoma na “inapotosha.”
Hata hivyo, baadhi ya mambo aliyoeleza Prof Mbarawa ikiwemo uwepo wa kituo cha zimamoto chenye waokoaji 10 wanaofanya shughuli za uokozi wa ardhini, hali ya uwanja wa ndege wa Bukoba na namna hali ya hewa ilivyokuwa wakati wa ajali vinafanana na yale yaliyoandikwa katika ripoti hiyo iliyokanwa na Serikali.
Zinazohusiana
Waliofariki ajali ya ndege Ziwa Victoria wanaagwa leo
ACT-Wazalendo yataka viongozi kuwajibika
Mapema leo asubuhi Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo aliwataka viongozi wanaohusika na ajali hiyo wawajibike na iwapo watashindwa kufanya hivyo angalau waombe radhi kwa umma kwa kile kilichotokea.
Kuhusu mjadala wa nani alifungua mlango ambao umekuwa ukihusishwa zaidi na kijana Majaliwa Jackson, Prof Mbarawa amesema mlango huo ulifunguliwa na mhudumu wa ndege baada ya kupata ujasiri wa kuona msaada wa nje.
‘Mhudumu alifungua mlango wa ndege’
“Wananchi waliokuwa wanafanya shughuli za uvuvi walifanya juhudi za kufungua mlango kwa nje, hali hiyo ilimpa ujasiri mhudumu wa ndege na abiria kufungua mlango huo baada ya kubaini nje kuna msaada unaoweza kuwasaidia,” amesema.
Awali kijana Majaliwa Jackson ambaye ni mvuvi alitajwa kuwa alihusika kufungua mlango wa ndege jambo lililoibua sintofahamu kwa baadhi ya watu kuhoji uwezekano wa mlango kufunguliwa kutokea nje.
Kijana huyo ambae yeye na wenzake walishiriki katika zoezi la uokoaji amejiunga na Jeshi la Zima moto na Uokozi kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango alioutoa.