Ripoti: Watanzania 9 kati ya 10 wanatumia miguu kama nyenzo ya usafiri

January 27, 2023 7:25 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi ya wanaotumia miguu kama nyenzo ya usafiri imeongezeka kwa asilimia 0.6.
  • Ni kwa mujibu wa Utafiti wa Hali ya Kaya Tanzania (NPS) ya mwaka 2020-21.
  • Wataalamu wa afya wasema kuna faida lukuki za kutembea kwa miguu.

Dar es Salaam. Ndio! Huenda athari za kiafya zitokanazo na kutotembea kwa miguu mara kwa mara zikaendelea kupungua kwa Watanzania mara baada ya ripoti mpya kuonyesha asilimia 92.6 ya Watanzania wanatumia miguu kama nyenzo kuu ya usafiri.

Hiyo ni kumaanisha kuwa ni Watanzania tisa kati ya 10, hutumia miguu katika safari zao kuelekea katika shughuli mbalimbali za maendeleo. Idadi hiyo imeongezeka kidogo kutoka asilimia 92 ya mwaka 2014/15.

Ripoti ya Utafiti wa Kufuatilia Hali ya Kaya Tanzania (NPS ) ya mwaka 2020/21 ambayo imetolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Januari 17 mwaka huu imebainisha hayo katika kipengele cha nyanja za usafiri wa Watanzania.

Watu waishio vijijini ndiyo wanatumia zaidi miguu kuliko waishio mjini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 96.9 ya watu waishio vijijini husafiri kwa miguu wakati wa mjini ni asilimia 82.4.

Mathalan, katika jiji la Dar es Salaam, asilimia 68 ya watu wake hutumia miguu kama nyenzo kuu ya usafiri. 

Wakati idadi ya wanaotembea kwa miguu ikiongezeka kwa asilimia 0.6 kwa miaka nane sasa, idadi ya wanaotumia usafiri wa baiskeli imeshuka kutoka asilimia 2.5 mwaka 2014/15 mpaka asilimia 1.1 mwaka 2020/21.

Hiyo inamaanisha kuwa Mtanzania mmoja tu kati ya 10 ndiyo hutumia baskeli kwa usafiri.

Si watumiaji wa baiskeli pekee waliopungua,  Watanzania wanaotumia magari binafsi nao wamepungua hadi asilimia 0.6 mwaka 2020/21 ambapo mwaka 2014/15 walikuwa asilimia 0.8.

Upungufu umeonekana pia kwa watumiaji wa usafiri wa umma kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 3.7, ingawa matumizi ya magari ya shule (mabasi) yameongezeka kutoka asilimia 0 mwaka 2014/15 mpaka asilimia 1.5, mwaka 2020/21.

Ongezeko hilo la matumizi ya magari ya shule kama nyenzo ya usafiri limeripotiwa zaidi katika maeneo ya mjini hususani jijini Dar es Salaam ambapo matumizi ya usafiri huo ni asilimia 5.6.

Kutokana na jiji hilo kuwa na shule nyingi za binafsi ambazo ziko mbali na makazi ya watu, wazazi hulazimika kutumia magari ya shule kuwasafirisha watoto ili waende kupata elimu, licha ya kuwa wapo baadhi ya wanafunzi wanaotembea umbali mrefu au kutumia daladala. 

“Matumizi ya usafiri wa umma (mabasi) kama nyenzo ya usafiri wa kwenda na kurudi shule yamepungua kutoka asilimia 27 mwaka 2014/15 mpaka asilimia 23.2 mwaka 2020/21,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo 

Ripoti hiyo imeendelea kuainisha kuwa matumizi ya pikipiki nayo yameshuka kwa asilimia 0.1 hadi 0.4 wakati Watanzania wanaotumia nyenzo nyingine za usafiri ikiwemo ndege wakiripotiwa kuwa asilimia 0.1.


Soma zaidi


Kuna faida za kutembea

Huenda ikawa inachukuliwa kama jambo la ajabu lakini kuna faida lukuki za kiafya zitokanazo na mtu kutembea. Tovuti ya Better Health ya nchini Australia wanashauri ili kuwa na afya bora ni vema kutembea angalau kwa muda wa dakika 30 kila siku.

“Unapotembea unabeba uzito wako wa mwili, hii huboresha afya yako ya moyo pamoja na mapafu, utaweza kuepuka na ugonjwa wa kiharusi, vile vile kudhibiti shinikizo la damu, kutembea huimarisha mifupa na kuweka uwiano wa sukari mwilini, “ inaeleza tovuti hiyo.

Kiuchumi haijakaa sawa

Wakati kutembea kukiongeza faida katika mwili, lakini jambo hilo lina athari hasi kiuchumi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Dk Isack Safari  ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa uchumi hautakuwa kwa kasi kwani watu wengi wanatumia mda mwingi kutembea badala ya kuzalisha.

“Unapotembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine hauzalishi chochote, muda unaotumika kutembea ulipaswa kutumika kwenye shughuli za uzalishaji na hiyo ingechochea uchumi kukua kwa kasi,” amesema Dk Safari.

Safari ameongeza kuwa hali hiyo inatokana na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya watu katika maeneo ya vijijini ambako bado miundombinu ya kutumia magari binafsi au usafiri wa umma si rafiki.

Hata hivyo, ameshauri kuwa kuongeza shughuli za uzalishaji, pamoja na kubadili fikra kuwa kumiliki gari ni anasa vinaweza kusaidia kukua kiuchumi na kupunguza idadi ya watu wanaotumia miguu kama nyenzo ya usafiri.


Tangazo


Enable Notifications OK No thanks