Zingatia haya unaponunua simu kwa ajili ya kazi, biashara yako
- Mahitaji ya simu yanatofautiana kulingana na kazi na taaluma za watu.
- Simu itakayomfaa mtengeneza maudhui inaweza kuwa mzigo kwa mwanasheria
- Unahitaji kufanya utafiti kabla ya kununua simu ili iendane na taaluma yako.
Dar es Salaam. Ni kitu gani ambacho unazingatia wakati unaenda dukani au mtandaoni kununua simu janja? Vijana wengi huangalia uwezo wa uhifadhi (storage) huku wengine wakiangalia uwezo wa kamera na wengine wakinunua kile ambacho mfuko wao unaruhusu.
Wakati wengine wakiangazia bora mawasiliano, yapo mahitaji ya kina ambayo watu wengine hufuatilia wanaponunua simu kwani mbali na simu kuwika sokoni, huenda ikawa haikusaidii chochote katika kazi zako.
Mfano, wapo wachoraji ambao simu isiyo na kalamu haiwezi kuwasaidia lakini pia wapo watu wa muziki ambao simu isiyo na mfumo mzuri wa sauti haina maana kwao.
Fahamu kundi lako, kazi yako na mahitaji yako na kisha unaweza kutumia dondoo hizi pale unaponunua simu janja kwa ajili ya matumizi yako binafsi au ya ofisi:
Mtengeneza maudhui
Kwa mtengeneza maudhui, swali la kujiuliza ni maudhui gani unayotengenza? Baada ya hilo, fuata dondoo hizi.
Kama unafanya maudhui yanayohusisha sauti pekee yaani “Podcasts” na mengineyo, basi unahitaji simu yenye kung’amua sauti kwa hali ya juu. Simu kama Samsung Galaxy S9, LG V30 na Razer Phone ndiyo simu zitakazokufaa kwani simu hizi zina uwezo mkubwa wa kung’amua na kuchuuja sauti.
Inawezekana baadhi watu wakasema simu za Apple, ndiyo babu kubwa kwa sababu zimeshika masikio ya wengi lakini siyo watu wote wenye uwezo wa kumudu bei yake na hata masharti yake wakati wa kuzitumia.
Mbali na kamera nzuri, simu hizi zina uwezo mzuri wa sauti. Picha| Mtandao
Lakini ili uipate Samsung Galaxy S9, LG V30 na Razer Phone, hakikisha mfuko wako usipungue unene wa Sh1.8 milioni.
Kwa wadau wa maudhui ya video, simu ya Iphone 11 pro yenye uhifadhi wa 64GB inayouzwa Sh3.8 milioni yenye ukubwa wa 256GB inayouzwa Sh4.1 milioni ndiyo chaguo zuri kwako.
Mbali na kamera nzuri, simu hizi zina uwezo mzuri wa sauti japo uhamishaji wa video zako kwenda kwenye bidhaa zisizo za Apple utakuwia shida.
Msafiri
Mtandao wa travel budget umeainisha simu ya Iphone 11 kutwaa taji la kipengele hiki kwa sababu kamera ya mbele na nyuma ipo vizuri kama utapenda kupiga picha pale uwapo safarini. Simu hiyo inapatikana kuanzia Sh1.6 milioni kwa bei za nchini Marekani,
Hata hivyo Samsung note 10 hawajakaa nyuma kwa kuchukua nafasi ya pili huku Google pixel 3a wakichukua nafasi ya tatu.
Kama hupendi matoleo hayo, bado unaweza kuchagua kutoka One plus7 pro (Sh1.5 milioni), Motorolla G7 zinazouzwa kwa takriban Sh570,000 na Alcatel 1x kama pesa yako haija vuka Sh laki tatu.
Zinazohusiana:
- Simu za mkononi sasa kupima ugonjwa wa kifua kikuu
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
- Samsung, Huawei zinavyochuana katika soko la simu duniani.
Mpenzi wa michezo ya kidijitali (Gamer)
Orodha hii imetawala majina mapya ambayo wengi wanaweza kujiuliza. Black Shark 2, Asus ROG na Razer Phone 2 ni simu zitakazokufaa kama unatengeneza michezo ya simu na kama ni mchezaji wa michezo hiyo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Techadvisor, Asus Rog ina betri yenye uwezo wa 6000mAh inaongoza orodha hii na kufuatiwa na Red Magic 3s ambayo spika kubwa (stero speakers) zinapatikana mbele na siyo nyuma kama simu zingine.
Kama unatafuta simu ya tatu, Black Shark 2 ni simu ambayo inaambatana na vifaa vya uchezaji “magemu” hata hivyo, vifaa hivyo vinauzwa kivyake na bei yake siyo ya kitoto.
Black Shark 2 ni kati ya simu ambayo gamer yeyote anaweza furahia. Picha|Mtandao.
Wanaopenda kusoma na kuandika
Kwa haraka unaweza mshauri mwanasheria au mwalimu na mtafsiri taarifa kuchukua “Ipad” au tableti (Tablet) lakini taaluma hiyo inaenda mbali zaidi kwa sababu inaweza kumletea mtu changamoto ya kubeba kwa sababu vifaa hivyo ni vikubwa kuliko simu za kawaida.
Skrini kubwa, uhifadhi wa kutosha, mwanga usioumiza macho na uwezo wa kuchangamana na anachosoma ni vitu kadhaa vya kuangalia.
Hivyo hali hiyo inamuacha mtumiaji huyo kufikiria simu za Samsung toleo la Note kwani zina skrini kubwa na hata kalamu zake zinafaa kwa kuandikia na kuchangamana na vitu ambavyo msomaji anasoma.
Mbali na hapo, simu za LG toleo la V ni nzuri kutokana na ukubwa wa skrini yake na viambatanishi vya kutumia pamoja na simu kama “screen snipping” na uwezo wa kugawanya simu mara mbili. Unahitaji walau Laki tano kumiliki simu hizo.
Mfanya biashara
Mbali na muonekano, mfanyabiashara pia anatakiwa kuzingatia simu yake kwa ajili ya kuboresha huduma zake. Mfano kama unafanya biashara ya mtandaoni, unahitaji simu yenye intaneti nzuri kama Huawei Mate pro, Lg V50 na Samsung S 10 ambazo zina uwezo wa 5G.
Mbali na hapo unaweza tazamia simu zenye uwezo wa kutumia laini mbili kama Huawei P30 na One plus 7 pro zinaweza kuwa chaguo sahihi. Hili litakuondola kero ya kubeba simu mbili na kulazimika kuhamisha laini kila mara unaposafiri.
Matumizi ya simu ni zaidi ya mawasiliano. Kutumia simu kunaenda mbali na gharama na matoleo ya simu hivyo ni vizuri kufanya utafiti juu ya taaluma yako na kug’amua simu gani inafaa kwa matumizi yako ya kila siku.