WHO yazionya kampuni za tumbaku zinazofadhili matamasha ya kimataifa

August 16, 2019 8:16 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imezitaka Serikali kupiga marufuku matangazo, uchangishaji na ufadhili wa bidhaa za tumbaku katika matamasha na mikutano ya kimataifa.
  • Serikali zimetakiwa zichukue hatua za kupunguza idadi ya watu wanaoanza au kuendelea kuvuta sigara, kuchagiza afya na kulinda vizazi vijavyo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limezitaka Serikali kupiga marufuku matangazo, uchangishaji na ufadhili wa bidhaa za tumbaku katika matamasha na mikutano ya kimataifa ili kupunguza kasi ya uuzaji wa sigara ambazo husababisha magonjwa na vifo kwa wakazi wa dunia. 

Baadhi ya nchi za Umoja wa Mataifa (UN) zinatekeleza mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa bidhaa za tumbaku (FCTC) ambao unazitaka nchi wanachama kuchukua hatua mbalimbali kupunguza matumizi ya bidhaa hiyo.  

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na WHO imesema ni lazima dunia ishikamane kukomesha mkakati wa sekta ya tumbaku wa kuuza bidhaa zake ambazo husababisha uraibu, maradhi na vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka.

“Wito huu umekuja tena kufufuatia taarifa kwamba makampuni ya tumbaku yanadhamiria kuanzisha ushirika mpya na Serikali ili kufadhili matukio, mikutano au matamasha ya kimataifa katika nchi ambayo tayari iliridhia mkataba wa WHO wa kudhibiti tumbaku (FCTC),” inaeleza sehemu ya taarifa. 

Inadaiwa kuwa kampuni ya kimataifa ya sigara ya Philip Morris (PMI) hivi karibuni imetangaza ushirika na Uswisi ili kufadhili  banda la nchi hiyo mjini Dubai nchini Falme za Kiarabu, wakati wa tamasha la kimataifa la Expo 2020.

Kutokana na madai hayo, Serikali ya Uswisi imeamua kutokubali ufadhili huo hatua ambayo imepongezwa na WHO ambapo imetakiwa Uswisi kuridhia mkataba wa FCTC kwani nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa ambayo bado hayajafanya hivyo.


Zinazohusiana: 


Moja ya vipengele vya mkataba huo vinataka Serikali kuchukua hatua za kulinda afya ya umma kwa sera mbalimbali za kudhibiti matakwa ya makampuni ya bidhaa za tumbaku.

Taarifa hiyo ya WHO inaeleza kuwa kuruhusiwa kwa makampuni ambayo yanaongoza duniani kwa uzalishaji wa bidhaa za tumbaku na sigara ni kinyume na kaulimbiu ya maonyesho hayo ya Dubai ya Expo 2020 ambayo ni “kuunganisha fikra, kuunda mustakbali bora.”

Aidha, imebainisha kuwa Serikali ni lazima zichukue hatua za kupunguza idadi ya watu wanaoanza au kuendelea kuvuta sigara, kuchagiza afya na kulinda vizazi vijavyo.

Tumbaku imekuwa zao muhimu la biashara kwa nchi ya Tanzania ambapo ni zao la pili linaloingiza fedha nyingi za kigeni baada ya korosho jambo linalovutia wawekezaji kujenga viwanda vya sigara nchini. 

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, tumbaku iliingizia Tanzania fedha za kigeni Sh609.6 bilioni. 

Enable Notifications OK No thanks