Wanazuoni wamuenzi Prof Hirji, mtaalam wa takwimu za kitabibu
Prof Marjorie Mbilinyi akitoa mada wakati wa kongamano la kumuenzi mtunzi wa vitabu, Prof Karim Hirji jana jijini Dar es Salaam. Picha|Zahara Tunda.
- Mchango wake umegusa maeneo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo tasnia ya habari za takwimu.
- Ni mwandishi mzuri ambaye ameandika vitabu na maandiko mbalimbali zaidi ya 120 katika maisha ya kitaaluma yake.
- Wanazuoni washauri vijana kuiga mfano wake kusema kweli na kuitumikia jamii kwa weledi.
Dar es Salaam. Wanazuoni na wasomi wa vyuo vikuu wamemuenzi Profesa Karim Hirji aliyebobea katika masuala ya takwimu za kitabibu kutokana na mchango wake kitaaluma na ukuaji wa tasnia ya habari nchini.
Prof Hirji ni mwandishi mzuri ambaye ameandika vitabu na maandiko mbalimbali zaidi ya 120 katika maisha yake ya kitaaluma.
Amefundisha vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa muda wa miaka 40, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha California huko Marekani.
Mchango wa Prof Hirji katika tasnia ya habari unadhihirika katika kitabu chake cha Takwimu katika Uandishi (Statistics in the Media: Learning from Practice (2012) ambacho ni mahususi kuwasaidia waandishi wa habari kuripoti kwa usahihi habari za takwimu.
Kongamano hilo la kumuenzi Prof Hirji limefanyika jana (Januari 10, 2019) jijini Dar es Salaam ambapo wanazuoni hao wamesema mchango wake unajidhihirisha katika sekta mbalimbali lakini muhimu ni msimamo wake wa kusema ukweli.
“Kupitia kitabu chake cha Takwimu katika Uandishi unajifunza kwa vitendo na mifano na unaona ili mwandishi awe mgunduzi na mtafiti lazima utakutana na takwimu,” amesema Nizar Visram , mwandishi wa habari wa kujitegemea.
Zinazohusiana:
- Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
- Veronica Sarungi: TO anayeishi ndoto, taaluma ya ualimu
- Idrisa Magesa: Kijana aliyerithi mikoba ya kuuza uji kutoka kwa bibi yake
Vijana ambao wako masomoni wanamchukulia Prof. Hirji kama kioo cha kujitazama hasa wanapopanga mipango yao ya kuendesha maisha ikiwemo kujishughulisha katika kazi mbalimbali za kuingiza kipato.
“Mimi nilichojifunza kwa Profesa ni kwamba unaweza kufanya jambo zaidi ya moja kwenye taaluma yako, licha ya kubobea katika takwimu za kitabibu ameweza kutoa kitabu cha kuwasaidia waandishi hasa katika matumizi ya takwimu,” amesema Joel Ntile, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Pamoja na hayo Prof Karim Hirji amekuwa ni mwanazuoni anayewavutia wasomi kutokana na uthubutu wa kuisaidia jamii kwa kutoa machapisho yanayolenga kuelimisha na kuleta mabadiliko chanya.
Chambi Chachage ambaye ni mtafiti wa masuala ya Afrika kutoka Chuo Kikuu cha Princeton cha Marekani ameiambia Nukta kuwa alichojifunza kwa Prof Hirji ni umakini wake katika uandishi wa vitabu unaozingatia tafiti na vyanzo vya uhakika vya taarifa.
Amewataka wanahabari hasa waliojikita katika uchambuzi na data kutumia takwimu vizuri zinazotolewa na mamlaka husika ili kuleta matokeo chanya kwenye jamii.
“Ukiwa Mwandishi wa habari makini na taarifa zako ziko sahihi na zimechambuliwa vizuri, unaweza usiwe maarufu sana lakini mwisho wa siku ule ukweli wako utasimama na sio propaganda zinazopitapita tu,” amesema Chachage.