Wakulima wapewa changamoto kuongeza uzalishaji zao la mkonge

July 20, 2019 6:41 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali imesema kuna soko la uhakika la ndani na nje ya nchi. 
  • Wametakiwa kutafuta maeneo ili walime zao hilo na kuuza kwa viwanda vya ndani. 

Dar es Salaam. Wananchi wa Wilaya ya Same mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya wilayani humo kwa kuongeza uzalishaji wa zao la mkonge ili kujipatia soko la ndani na nje. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi hao wajipange na kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili waanze kulima mkonge ambao watakuwa wanauza kwenye kiwanda hicho.

“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji jirani ingieni kwenye kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na nje ya nchi. Tafuteni maeneo ya ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha mkonge sasa. Zao hili lipo kwenye mazao ya nyongeza ya mkakati ambayo ni chikichi na mkonge.

“Na uzuri wake unalima mara moja tu, halafu kila mwaka unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji simamieni jambo hili,” amesema Majaliwa wakati alipotembelea kiwanda hicho jana (Julai 19, 2019). 

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na korosho.

Kiwanda hicho kinahudumiwa na mashamba ya mkonge ya Hasani yenye hekali 2,453 yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Entreprises Tanzania Limited (METL). 


Zinazohusiana:


Meneja wa mashamba hayo, Ndekiwa Nyari amesema uzalishaji wa mkonge umekuwa ukiongezeka kidogo kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani za mkonge 713 na hadi kufikia mwaka 2018 walifikisha tani 890 za mkonge.

“Mwaka huu tunatarajia kufikisha tani 1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge limeongezeka,” amesema.

Amesema moja ya changamoto inayowasumbua ni tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge ambao haujakomaa, hali ambayo inaua miche hiyo michanga.

Pia ukosefu wa maji ya uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha singa za katani ambazo ni safi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema atamtuma Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aende Makanya akatatue kero za wafanyakazi wa kiwanda na mashamba hayo. 

“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, maana watumishi wameweka malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona wanaoendesha mitambo hawana ‘gloves’, wengine wamevaa kandambili badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu…” amesisitiza Waziri Mkuu.

Majaliwa leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea Wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa ameshika katani  iliyokua imeanikwa, wakati alipotembelea shamba la katani la Hassan Sisal Estate Makanya, wilayani Same katika mkoa Kilimanjaro Julai 19.2019. Anayetoa maelezo ni Meneja Mshauri wa shamba hilo, Ndekirwa Nyari. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Enable Notifications OK No thanks