Wafanyabiashara wanavyoweza kunufaika na kalenda ya Twitter

Mwandishi Wetu 0828Hrs   Julai 03, 2019 Teknolojia
  • Mtandao huo umetoa kalenda inayoainisha matukio makubwa yatakayofanyika duniani Julai mwaka huu.
  • Matukio yanatarajiwa kuleta mijadala kwa wafuasi wa mtandao huo. 
  • Mijadala hiyo inaweza kufungua fursa za biashara, kampeni na kufahamiana na watu.

Kama hukutumia vizuri robo ya pili ya mwaka 2019 kutangaza biashara yako mtandaoni, basi Twitter wamekuletea fursa nyingine ya kalenda ya matukio makubwa yatakayofanyika duniani Julai mwaka huu. 

Matukio hayo yanaweza kukusaidia kuongeza idadi ya wafuasi na hata kuwafikia watu wengi zaidi, ikizingatiwa kuwa yatatawala kwa sehemu kubwa mijadala katika mtandao huo. 

Taarifa ya mtandao huo iliyotolewa Julai 1, 2019 inaeleza kuwa kalenda hiyo inaonyesha tarehe, tukio husika na mahali litakapofanyika. Pia inaweka takwimu za watu walioshiriki mjadala wa tukio husika kwa miaka iliyopita. 

Kalenda hiyo ambayo ni sehemu ya kalenda ya mwaka mzima inaweza kuwa msaada kwa kampeni, maudhui na hata matangazo ya kibiashara kuvutia watu kutumia huduma na bidhaa mbalimbali. 

Pia inasaidia kujua ni mjadala gani unavuta watu wengi na fursa za masoko zilizojificha katika mjadala hiyo ambazo zikitumika zinaweza kufungua mlango wa kunufaika kwa njia mbalimbali. 

Kwa wale ambao Twitter ndiyo kila kitu, basi ni fursa nyingine ya kushiriki mijadala ili kujulikana na kukutana na watu wapya ambao wanaweza kuwa chanzo cha fursa mbalimbali ikiwemo masomo na biashara. 

“Kutoka michezo hadi sayansi na teknolojia, mwezi Julai ni mijadala kwa kila mtu. Hizi ndiyo tarehe na mijadala muhimu ya kuifikiria wakati ukiweka mipango yako ya maudhui mwezi huu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 




Baadhi ya matukio makubwa ambayo yanatarajia kuteka mijadala ya mtandao huo ni siku ya uhuru wa Marekani ambayo itafanyika kesho Julai 4. 

Siku hii ni muhimu kwa Wamarekani ikizingatiwa kuwa Taifa hilo limekuwa na historia ya muda mrefu lakini lina nguvu kubwa ya kiuchumi duniani. 


Zinazohusiana:


Tukio lingine litakuwa ni Siku ya Emoji Duniani ambayo itafanyika Julai 17. Siku hiyo ni muhimu kwa sababu emoji (alama na stika) zimekuwa zikitumika kufanikisha na kurahisisha mawasiliano kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii. 

Hata hivyo, kalenda iliyotolewa na Twitter inatoa somo kwa kila mtu kuishi kwa mipango na kujitengenezea kalenda binafsi inayoonyesha mambo atakayoyafanya ili kuepuka mgongano wa majukumu katika maisha yake. 

Kwa kutumia huduma ya Google kalenda unaweza kupanga mipango yako vizuri na siku ya tukio fulani ikifika, kupitia simu au kompyuta yako utataarifiwa na kukumbushwa.

Related Post