Vodacom kuingiza sokoni mashine za kidijitali za kuuzia vinywaji, vitafunio

December 2, 2019 9:13 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Itakuwa inatumia mfumo wa malipo kwa njia ya simu wa M-Pesa.
  • Baada ya mteja kulipa bidhaa anayotaka, mashine inampa bidhaa moja kwa moja.
  • Ni muendelezo wa ATM za maziwa ambazo zinafanya kazi nchini. 

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania imesema inakusudia kuingiza sokoni mashine ya kuuzia vitafunio na vinywaji iliyoungaanishwa na mfumo wa malipo kwa njia ya simu wa M-Pesa, hatua itakayopunguza utegemezi wa vioski na maduka kununua bidhaa ambayo hufungwa nyakati za usiku. 

Mashine hiyo ambayo hutambulika kama “Vending Machine” ni mashine ya moja kwa moja ambayo hutoa vitu kama vile vitafunio, vinywaji, sigara na tiketi za bahati nasibu baada ya watumiaji kuingiza pesa, kadi ya mkopo, au kadi iliyoundwa maalum kulipia bidhaa husika. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hisham Hendi ameeleza katika ukurasa wake wa Twitter leo (Desemba 2, 2019) kuwa mashine hiyo itakuwa ya kwanza nchini Tanzania ambayo itakuwa inapokea malipo kwa kutumia M-Pesa na itaingia sokoni hivi karibuni. 

Hata hivyo, Vodacom haijaweka bayana tarehe kamili itakapoziingiza mashine hizo soko na mahali watakapoanzia kuzifunga nchini. 

“Sisi ni wa kwanza kuleta teknolojia hii Tanzania na ni mashine ya kwanza ya kuuzia inayofanya kazi kupitia M-Pesa,” amesema Hendi katika ukurasa wake wa Twitter. 

As always we bring new M-Pesa innovation, first vending machine in TANZANIA accepts payment via M-Pesa, soon in the market, watch! @VodacomTanzania
@Vodacom
@VodafoneGroup
@FSDTanzania
pic.twitter.com/cdChlQIbRV

Ameeleza kuwa ili mteja apate kinywaji au kitafunio kilichopo katika mashine hiyo, anatakiwa kuchagua bidhaa yenye namba maalum ambazo zimeunganishwa na mfumo wa “QR Code” kisha atatumia kamera ya simu janja ambayo ina skani msimbo (CODE)  na kisha kukamilisha malipo ndani ya muda mfupi.

Baada ya kukamilisha malipo kwa M-Pesa, bidhaa aliyochagua inatoka nje na anakuwa yuko tayari kuitumia. 

Mashine kama hizo ziko katika maeneo mbalimbali duniani ambapo kwa sasa Tanzania ina mashine maalum (ATM) ya kuuzia maziwa mkoani Kilimanjaro ambayo imekuwa mkombozi kwa wafugaji kujipatia kipato. 

Wakati Vodacom ikitarajia kuzindua mashine hiyo, kwingineko duniani, teknolojia imeendelea kugonga vichwa ikiwemo ofa ya manunuzi ya “Cyber Monday”, Instagramu kueleza jinsi inavyotambua tabia za watumiaji wake na programu ya Google Maps inavyoongoza kwa kutumiwa na watu wengi kutafuta taarifa za kibiashara mtandaoni.

Unayotakiwa kufahamu kuhusu “Cyber Monday”

Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaofanya manunuzi ya bidhaa kwa njia ya mtandao, basi huenda leo ikawa siku njema kwako.

Kwa wanaofahamu leo Jumatatu ya Desemba 2, 2019 inajulikana kama “#CyberMonday” ambayo maduka ya mtandaoni hutoa ofa kubwa na kuuza bidhaa na huduma kwa bei ya chini sana kuliko matarajio ya mteja. 

Siku hii imekuwa ikitumiwa na watu mbalimbali duniani hasa katika nchi zilizoendelea kama Marekani na Uingereza kununua bidhaa kwa ajili ya maandalizi ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Kwa mujibu wa jarida la mtandaoni la Business Insider, Cyber Monday inaanza mapema saa 12:00 asubuhi na inaweza kudumu kwa wiki nzima ambapo maduka makubwa ya  mtandaoni duniani yakiwemo ya Ali Baba,  Amazon, Best Buy, na Walmart hutoa punguzo la bei kwa bidhaa mbalimbali ili kuvutia wateja wengi zaidi. 

Mathalani, katika duka la Amazon na Best Buy, televisheni aina ya  Vizio P-Series Quantum TV inauzwa kwa dola za Marekani 870 sawa na takriban Sh2 milioni kutoka bei ya kawaida ya dola 1,399.99 (takriban Sh3.2 milioni)


Soma zaidi:


Kwa kawaida, Cyber Monday hufanyika baada ya sikukuu ya shukurani (Thankgiving) na siku ya “Black Friday” ambayo ni mahususi kwa maduka duniani kutoa ofa na punguzo la bei ili kuwafaidisha watu wanaotafuta zawadi kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka. 

Aina hiyo ya manunuzi katika siku ya Cyber Monday ilianza mwaka 2005 kuwapa fursa watu kununua bidhaa popote walipo. Katika mitandao ya kijamii wanatumia zaidi neno #CyberMonday ili kuhamasisha watu kuifahamu zaidi. 

Instagram yaeleza inavutumia mashine kuwapa watumiaji wake wanachotaka

Mtandao wa kijamii wa Instagram umeeleza kuwa unatumia teknolojia ya mashine ya kusoma tabia za watumiaji wake (multiple machine learning (ML)) na kuwapa maudhui yanayoendana na kile wanachokipenda. 

Kwa mujibu wa taarifa ya kitaalam iliyotolewa na mtandao huo Novemba 25, 2019, zaidi ya nusu ya watumiaji wa Instagram wanatembeleaa kipengele cha kutafutia vitu (Instagram Explore) kupata picha, video na habari mpya zinazoendana na mapendeleo yao. 

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kupendekeza yanayofaa zaidi nje ya mabilioni ya chaguzi kwa wakati na kwa kiwango cha juu huleta changamoto nyingi za kujifunza mashine (ML) ambazo zinahitaji suluhisho la riwaya la uhandisi.

“Tulishughulikia changamoto hizi kwa kuunda safu ya lugha za maombi maalum, mbinu nyepesi za uandikaji, na zana zinazowezesha majaribio ya kasi ya juu. Mifumo hii inasaidia kiwango cha kuchunguza wakati wa kuongeza ufanisi wa mtaalam wa programu wa simu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Instagram inafanya hivyo ikiwa ni hatua kuboresha huduma zake na kuwa karibu na watumiaji wake. Picha|Mtandao.

Google Maps yatajwa kinara wa utafutaji wa taarifa za biashara mtandaoni

Utafiti mpya wa tabia za utafutaji vitu mtandaoni, umeitaja programu tumishi ya Google Maps kuwa inashika nafasi ya kwanza kutumiwa na watu kutafuta taarifa za kibiashara ili kufanya manunuzi na kutembelea maduka yaliyo karibu na maeneo wanayoishi.

Ripoti ya utafiti huo uliopewa jila la “Brandify Local Search Consumer Survey” uliofanyika nchini Marekani imebaini kuwa robo tatu au asilimia 77 ya watu 1,000 waliohojiwa walisema wanatumia zaidi Google Maps kutafuta taarifa za kibiashara. 

Programu zingine zinatumika kutafuta taarifa za kibiashara ni pamoja na Facebook kwa asilimia 38, mtandao wa Yepi (asilimia 35), tovuti za biashara (asilimia 32). 

Pia, ripoti hiyo iliyotolewa wiki iliyopita inaeleza kuwa wanaotafuta taarifa hizo hutumia zaidi simu janja kwa asilimia 81 wakifuatiwa na watumiaji wa kompyuta mpakato na tableti. 

Lakini wengi wanaotumia programu hizo kutafuta taarifa za kibiashara hufanya hivyo zaidi wakiwa nyumbani na kwa sehemu hufanya wakiwa kwenye magari, kazini na safarini. 

Katika hatua, nyingine ripoti hiyo inaeleza kuwa baada ya mtu kupata taarifa anazozihitaji hatua ya kwanza na ambayo hutumika zaidi ni kutembelea eneo la biashara (duka la bidhaa au huduma) na wengine hupiga simu kwa wahusika na kundi la mwisho hutumia barua pepe au mitandao ya kijamii kupata taarifa zaidi. 

Enable Notifications OK No thanks