Uunganishwaji wa WhatsApp, Facebook na Instagram bado sana

February 14, 2019 4:19 pm · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Mark Zuckerberg amesema mabadiliko hayo yapo katika hatua za mwanzo za utekelezaji na kwamba huenda yakaanza kuonekana machoni mwa watu angalau mwaka 2020 au zaidi.
  • Miongoni mwa maswali magumu kwa sasa ni je, baada ya uunganishwaji wa mitandao hiyo usalama wa watumiaji wake wanaokadiriwa kufika bilioni 2.6 utakuwaje?
  • Sasa mfanyabiashara ataweza kuwafikia watumiaji wa mitandao yote kwa wakati mmoja.

Mtandao wa kijamii wa Facebook umesema utaendelea na mpango wake wa kuunganisha majukwaa yake ya Facebook, Instagram na WhatsApp katika jukwaa moja la mawasiliano na kubainisha kuwa mchakato wa hatua hiyo utachukua muda kidogo tofauti na matarajio ya wengi.

Mwanzilishi mwenza na mmiliki wa mitandao hiyo Mark Zuckerberg amesema mabadiliko hayo yapo katika hatua za mwanzo za utekelezaji na huenda yakaanza kuonekana machoni mwa watu angalau mwaka 2020 au zaidi.

Kauli hiyo ya kigogo huyo wa juu wa Facebook inafuta matarajio au hofu ya wengi kuwa huenda kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Marekani ingefanya mabadiliko hayo katika miezi ya hivi karibuni.

Hayo yakifanyika yatakuwa maendeleo makubwa hasa kwa mitandao ya kijamiii kwa watu wataweza kutumiana jumbe kutoka majukwaa matatu tofauti kwa wakati huo huo bila kujali mtumiaji aliingia kutumia jukwaa gani la mtandao wa kijamii.

Gazeti la The New York Times la Marekani limeinukuu Facebook ikisema,  “Wanajitahidi kujenga jukwaa bora ambalo litaweza  kutumiana ujumbe kwa ubora na wanaweza kufanya hivyo. Pia, watu wanataka ujumbe kuwa wa haraka, rahisi, na kuaminika na bila kusahau faragha.”

“Tunajitahidi kufanya zaidi bidhaa zetu kuwa na faragha na kuzuiwa kudukuliwa (end to end encrypted)  na kuzingatia iwe rahisi kufikia marafiki na familia kwenye mitandao,” Facebook imenukuliwa zaidi na gazeti hilo.

Pia mabadiliko hayo sasa yanaweza kuleta fursa kubwa ya kibiashara miongoni mwa watumiaji  wake wanaokadiriwa kufikia bilioni 2.6 duniani.


Zinazohusiana: 


Mabadiliko hayo yatakuwa ni fursa kwa wafabiashara kuwafikia wateja kwa kuwa sasa mfanyabisahara ataweza kutuma ujumbe wake kwenye mitandao mitatu ya kijamii kutoka kwenye mtandao mmoja.

Kwa mantiki hiyo wataweza kuwafikia watumiaji wengi duniani kote bila kujali rika kuanzia wale wa miaka 16 hadi 24  ambao wapo zaidi kwenye instagram na Whatsapp pamoja na watumiaji wa kuanzia miaka 25 na kuendelea ambao wengi wao wapo kwenye Facebook.

Kitendo hicho cha kuunganisha mitandao hiyo itapelekea pia meseji za kibishara kupelekwa kirahisi kwa wateja ukilinganisha na sasa.

Uamuzi huo wa Facebook inayomiliki mitandao ya WhatsApp, Instagram na Facebook, utaleta ushindani kwa kampuni zinazotoa huduma za baruapepe katika masuala ya masoko ambazo zimetawala soko hilo kwa muda mrefu sasa.

Tovuti ya mtandao wa Social Media Today inaeleza kuwa wastani wa kuonwa kwa  barua pepe hizo za masoko ni asilimia 20 wakati ule wa kufungua (bofya) baruapepe hiyo inapotumwa kwa wateja ni asilimia 2.3.

Kupitia mabadiliko hayo, sasa meseji za kibiashara zinaweza kuonwa kati ya asilimia 60 mpaka 80 huku uwezekano wa kuifungua (kubofya) ukiongezeka kwa zaidi ya mara nne au 10 zaidi ya ule wa barua pepe.

Facebook ikifanikiwa kuunganisha mitandao hiyo italeta changamoto kubwa zaidi kibiashara katika utumaji ujumbe hususani kwa mtandao kama wa WeChat wa China ambao nao hutumika  karibu na mitandao yote nchini humo kutuma meseji za kibiashara kwa watumiaji bilioni 1.08.

Wakati mabadiliko hayo yanatarajiwa kutokea swali kubwa linabaki ni kwa kiasia gani mabadiliko hayo yatalinda faragha za watumiaji wake ulimwenguni ikiwemo milioni 6.1 wa Facebook Tanzania ambao wanakadiriwa kuwepo hadi Desemba 2017 kwa mujibu wa mtandao wa Internet World Stats. 

Hadi sasa Facebook wanaendelea kutafunwa na kashfa mfululizo za usalama wa taarifa za watumiaji baada ya sakata la kuiba taarifa lililohusisha taasisi ya Cambridge Analytica kutoka Uingereza.

Enable Notifications OK No thanks