Ushindani nguo za mtumba, dukani unavyowafaidisha wanunuzi Tanzania
- Baadhi ya wanunuzi wamesema kuna muda hata mtu wa uchumi wa kati hawezi kuukwepa mtumba.
- Bei za nguo za dukani na ubora wake ni miongoni mwa mambo yanayoleta mjadala kwa Watanzania.
- Wabunifu wa mavazi nao wakimbilia malighafi za nje ya nchi.
Dar es Salaam. Jua la utosi, kelele zitokazo kwenye vipaza sauti vilivyopo kila kona ya soko, hazikumzuia Mziani Beka kutafuta mtandio wa ndoto zake.
Rundo la mitandio kwenye moja ya meza za wauza mitumba waliopo Kariakoo mtaa wa Msimbazi ilikuwa ni sehemu sahihi kwa Mziani kutafuta nguo hiyo ambayo hutumiwa zaidi na wanawake kujifunika kichwani.
Mama huyo aliingiza mkono wake kwenye rundo hilo akivuta mtandio aliouona unamvutia na kisha mtandio huo uliungana na mingine miwili iliyokuwa begani ikisubiri kulipiwa.
“Mitatu hii, shika hela yako,” Mziani aliyasema hayo akimwambia muuzaji huku akitoa noti mbiliza Sh2,000 na kurudishiwa buku iliyomridhisha na kisha kushika njia yake kuelekea katika shughuli zingine.
Mitumba, hizi ni bidhaa ambazo zimeshatumika na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali na hivyo husafirishwa kuja nchini ili kutumika tena kwa wenye uhitaji.
Bidhaa hizo ni pamoja na mavazi, vyombo, mashine na hata vifaa vya umeme.
Mama huyo ni mmoja kati ya maelfu ya Watanzania wanaotumia nguo za mtumba licha ya kuwepo kwa nguo nyingi mpya za madukani.
Wasichokijua wengi, mbali na sababu ya gharama, kuna sababu zingine zinazofanya masoko ya mitumba nchini Tanzania kujipatia soko licha ya jitihada mbalimbali za kuhamasisha uvaaji wa nguo dukani na zile zinazotengenezwa kwa malighafi za Tanzania.
Bidhaa hizo ni pamoja na mavazi, vyombo, mashine na hata vifaa vya umeme. Picha| Rodgers George.
Kwanini watu hupendelea nguo za mitumba?
Gharama nafuu ikilinganishwa na dukani
Sababu kubwa inayosemwa na wengi ni kuwa nguo za mitumba zina bei nafuu ikilinganishwa na nguo za dukani.
“Mtumbani unapata shati kali kwa Sh7,000, Sh10,000 hadi Sh15,000 shati kali tu ambalo dukani ni Sh35,000. Kwa bei hiyo mtumbani nina mashati 10,” ameeleza Kennedy William mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Kennedy, Sh7,000 ni kwa mashati yenye ubora wa juu, japo yapo hadi ya Sh3,000 na Sh2,000 ambayo pia ni mazuri na yapo sokoni.
Kupenda utofauti
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Shinuni Msoud ambaye kwenye kabati lake asilimia 70 ya nguo zake ni mtumba, amesema yeye huenda mitumbani kutafuta nguo ambayo atakuwa tofauti na umati wa watu wengine.
Binti Masoud amesema anaamini kuwa wasichana wengi hupendelea kununua mtumba ili wawe tofauti kwani nguo za madukani ukinunua ni kama umeamua kuvaa sare na wana Dar es Salaam.
“Kama unazifahamu sketi flani hivi mtindo wake ni kama sketi ambayo haijapigwa pasi, vaa hiyo kisha toka uone kama hujakutana na mapacha wenzako zaidi ya kumi. Lakini ukienda mtumbani, unaweza ukaishia kuulizwa hii nguo umeitoa wapi na kila mtu na usione mtu hata mmoja aliyefanana na wewe,” ameeleza Shinuni.
Utofauti huo, ndiyo unaompa furaha na kujiamini Shinuni kwa sababu kuvaa siyo tu kusitiri mwili bali kuwa na mwonekano mzuri mbele ya macho ya watu.
Soma zaidi
- Tumbaku: ‘Rafiki wa mashaka’ anayeiweka Tanzania njia panda
- Yatakayokupata usipodhibiti minyoo inayoshambulia mwili wako
- Mbinu zitakazokusaidia kutumia WhatsApp kwa urahisi
Uimara wa nguo za mitumba unasifika
Ni imani ya baadhi ya watu kuwa nguo za dukani kweli ni mpya lakini hazidumu kwani kiwango chake cha uimara ni cha chini. Kwa maana hiyo, huenda nguo za mtumba zikawa ni kimbilio la watu wengi ambao hawahitaji kununua nguo mara kwa mara kutokana na kuchakaa.
Kati ya watu hao ni Simon Mbutu ambaye ni Daktari wa mifugo jijini Dar es Salaam amesema hata ukiwa na uchumi wa kati kuna muda ambao mtumba “lazima ukuhusu” kwani hata dukani, unaweza ukachoshwa na ubora wa vitu vyake ikizingatiwa wengi hununua bidhaa zao ambazo zina muonekano mzuri lakini ubora wake ni wa chini.
“Kwa sisi wavivu wa kutembea, tunajua soko la nguo ni kariakoo, ukienda kule mzigo mkubwa umetoka China, sasa ‘shati la Mchina’ halikai muda mrefu unaishia kununua suruali za kitambaa au Cadet tu,” ameeleza Mbutu ambaye mvaaji mzuri wa tisheti, viatu na suruali aina ya ‘Jeans’.
Endapo tu Tanzania ingekuwa na uwezo wa kutengeneza nguo zenye ubora, “mambo yangekuwa supa sana”. Picha| Otilia Mtitu.
Madukani nako wanasemaje?
Angel Swalo ni mfanyabiashara mwenye duka la nguo Kariakoo jijini Dar es Salaam, amesema ubora wa nguo za dukani inategemeana na sehemu ambayo mtu amenunua mzigo wake.
“Zipo nchi ambazo zinafahamika kwa kuwa na nguo nzuri na ambazo malighafi yake hudumu kwa muda mrefu sema sasa nguo zake ni za gharama na kwa hapa Kariakoo, ukinunua mzigo unakaa sana,” amesema Swalo.
Akitolea mfano wa kipindi cha Corona ambapo alilazimika kuchagua nguo kwa njia ya mtandao na kisha kununua nguo bila hata kuyoana malighafi yake, Angel amesema wateja wengi walionyesha kutokuridhishwa na nguo hizo pale walipozishika tu.
“Zinakuwa yepesi. Hata hivyo, ukisema ukanunue nguo Uturuki au Thailand, Watanzania wengi hawawezi kuzimudu kwani zinakuwa na bei kubwa. Shati tu unaweza kuambaiwa Sh50,000 kwa Kariakoo hapa utakaa nalo dukani,” ameeleza Angel ambaye duka lake limesheheni mashati na fulana.
Angel amesema, endapo tu Tanzania ingekuwa na uwezo wa kutengeneza nguo zenye ubora, “mambo yangekuwa supa sana”.
Hata hivyo hilo litawezekanaje hata wabunifu wanapendelea kununua malighafi Na vitambaa kutoka nje ya nchi?
Usikae mbali na kurasa za Nukta kujua zaidi ni kwa nini wabunifu wanapendelea malighafi za nje ya nchi na siyo Tanzania kutengeneza nguo.