Mbinu zitakazokusaidia kutumia WhatsApp kwa urahisi
- Ni pamoja na kusoma na kuhifadhi meseji kwa matumizi ya baadaye.
- Unaweza kurekodi ujumbe wa sauti bila ulazima wa kushikilia skrini yako au simu.
- Mtandao huo unakuwezesha kuweka mawasiliano ya watu unaozungumza nao zaidi kuwa juu ya mawasiliano ya kawaida.
Dar es Salaam. Ikiwa na watu zaidi ya bilioni 5 waliyoipakua hadi sasa kwenye duka la mtandaoni la programu za simu la Play Store, WhatsApp ina mengi ya kukupa zikiwemo mbinu ambazo hujawahi kuzitumia tangu upakue programu hiyo kwenye simu yako.
WhatsApp ambayo kwa sasa iko chini ya mtandao wa Facebook na kiungo muhimu cha mawasiliano imefanya maboresho muhimu ambayo yanawasaidia watumiaji kutumia programu hiyo kwa urahisi zaidi. Mbinu hizo ni:
1. Kurekodi ujumbe wa sauti bila ulazima wa kushikilia skrini yako
Kwa watumiaji wa WhatsApp imezoeleweka kurekodi ujumbe wa sauti kwa kushikilia sehemu ya kurekodi kwenye skrini yako kabla ya kumtumia mtu.
Kwa sasa, unaweza kurekodi ujumbe huo kwa kubonyeza sehemu ya kurekodi mara moja na kuslaidi kuelekea juu (slide up) na hapo unaweza kurekodi ujumbe wako wa sauti huku ukiendelea na shughuli zingine.
Baada ya kumaliza kurekodi ujumbe wako,utume kwa kubonyeza “send”.
2. Kuhifadhi ujumbe muhimu
Huenda mara nyingi unapohitaji kupitia meseji zako za muhimu, unalazimika kusoma neno baada ya neno na kama umesahau ujumbe huo ulitoka kwa nani, basi hali inaweza kuwa tafrani zaidi.
Kama ulikuwa haufahamu, unaweza kuhifadhi ujumbe muhimu kwa kuuwekea alama ya nyota na kisha utaupata kwa kubonyeza menyu ya WhatsApp na kuchagua “Starred messages” yaani meseji zilizowekewa alama ya nyota na utakuta meseji yako hapo. Ni rahisi eeh!.
3. Baki mtandaoni bila kutumia simu yako
Inaweza ikawa ngumu kwako kutumia simu na kompyuta yako kwa wakati mmoja. Kama ulikuwa haufahamu, una uwezo wa kutumia WhatsApp yako kwenye komyuta bila hata ya kushika simu.
Unachotakiwa kufanya ni kuingia mtandaoni kwenye kompyuta yako na kutafuta “WhatsApp Web”. Ukiingia kwenye tovuti hiyo, utaombwa kuskani kodi kwa kutumia simu yako.
Hapo utabonyeza menyu ya WhatsApp ya kwenye simu yako na kisha utachagua sehemu ya “WhatsApp Web” na kisha utaskani msimbo (code) uliopo kwenye kompyuta yako. Hapo utatumia WhatsApp kwenye kompyuta yako.
Ukiingia kwenye tovuti hiyo, utaombwa kuskani kodi kwa kutumia simu yako. Picha| Freepik.com.
4. Soma meseji za WhatsApp bila ulazima wa kufungua App yako
Kuna wakati unaweza kuhitaji kusoma meseji ya mtu na usitake ajue kama umesoma. Mbali na kuondoa “bluetick” unaweza kusoma ujumbe wa WhatsApp kwenye skrini ya taarifa (notification bar) kwa kuslaidi kuelekea chini (slide down).
Hata hivyo, njia hii inaweza isifanye kazi kwa wale waliowasha matengenezo ya faragha (privacy settings) kwenye skrini ya taarifa.
Zinazohusiana
- WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
- WhatsApp yaongeza udhibiti kujiunga na makundi ya mtandao huo
- Unavyoweza kuokoa macho, chaji kwa “dark mode” ya WhatsApp
5. Kuweka rafiki na makundi sogozi juu ya chati zote
Bila shaka kuna watu ambao unawasiliana nao sana na haupendi kukosa ujumbe wowote wanaokutumia. Unaweza kutofautisha chati zao na za wengine kwa kuziweka juu ya chati zote. Yaani haijalishi meseji ngapi zitaingia baada ya ujumbe wake, meseji yake daima itabaki juu.
Mbinu hiyo inaitwa kupini jina la mawasiliano (pinning contact). Kufanya hivyo, bonyeza chati unayotaka “kuipin” na kisha bonyeza alama ya kipini itakayokuja juu.
Unaweza kufanya mambo mengi na WhatsApp yako ikiwemo kuzuia watu wasikuunge kwenye makundi bila ridhaa yako, na mengine mengi.
Je, ni mbinu gani ambayo unahisi wewe unaitumia na wengine hawaijui? Tuandikie kupitia editorial@nukta.co.tz au tutumie ujumbe kupitia WhatsApp kwa namba +255 677 088 088.